Customer Feedback Centre

Ministry of Health

KIGOMA KUPATA AMBULANCE 17 KWAAJILI YA KUBEBEA WAGONJWA

Posted on: July 10th, 2023

Na. WAF- KIGOMA

NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema kuwa, Mkoa wa Kigoma utapata magari ya kubebea wagonjwa 17 (Ambulance) zitazosaidia kutatua changamoto ya huduma za Rufaa na pamoja na vifo vya mama na mtoto katika Mkoa huo.

Dkt. Mollel alisema hayo alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma na maendeleo ya ujenzi wa miundombinu pamoja na upatikanaji wa vifaa tiba katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma.

Alisema, Serikali imenunua jumla ya magari ya kubebea wagonjwa 727 ambayo inatarajia kugawa nchi nzima, huku akibainisha kila Halmashauri inatarajia kupata magari mawili na hospitali ya Mkoa kipata gari moja hali itayosaidia kupunguza changamoto ya uhaba wa magari hayo katika Mkoa.

"Tumenunua Ambulance 727, na tayari Ambulance hizo zimeanza kuingia, na Tumekubaliana angalau zifike Ambulance 200, kuna uwezekano wa kila Halmashauri kupata Ambulance mbili na kila hospitali ya Mkoa kupata Ambulance, hivyo kuna uwezekano wa mkoa wako kupata Ambulance 17 zitazosaidia kupiga hatua katika huduma za Afya”, alisema.

Aidha, Dkt. Mollel aliwapongeza Watoa huduma wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni kwa jitihada na ubunifu wanaoendelea kuonesha katika kuboresha huduma kwa wananchi, hali iliyopelekea kupunguza Rufaa za wagonjwa ndani ya Mkoa huo kwa zaidi ya asilimia 28 ndani ya muda mfupi, huku malengo yakiwa kupunguza asilimia zaidi ya 90.

Katika kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za dawa katika hospitali hiyo Dkt. Mollel aliwataka viongozi wa hospitali hiyo kuhakikisha wanakuwa na Washitiri wazuri na wenye lengo la kuwasaidia wananchi kwa kufuata vigezo na taratibu zote ili kuhakikisha hakuna changamoto ya upungufu wa dawa katika vituo vyote vya kutolea huduma”, amesema,


Nae, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma (Maweni) Dkt. Binaga alisema Hospitali itaendelea kushirikiana na Serikali kuu kutenga fedha kwaajili ya maendeleo ya miradi mbalimbali inayoendelea katika hospitali hiyo ili kuhakikisha inamalizika kwa wakati na wananchi wanaanza kunufaika na huduma katika miradi hiyo.

Sambamba na hilo aliongeza, Hospitali inaendelea kutoa huduma kwa njia ya mikoba (outreach) inayowafuata wagonjwa katika jamii na kuwahudumia katika mazingira yao hali iliyosaidia kuboresha afya za wananchi.

Pia, alisema kutokana na kutoa huduma bora kwa wananchi, Hospitali imeendelea kupokea wagonjwa mbalimbali kutoka nje ya nchi ikiwemo nchi ya Burundi wanaofika kupata huduma kupitia hospitali hiyo ya Maweni.