Customer Feedback Centre

Ministry of Health

KAMPENI YA TAULO ZA KIKE MILIONI 5 KWA WANAFUNZI WALIPO SHULENI YAZINDULIWA.

Posted on: January 17th, 2024

Na. Majid Abdulkarim, Dodma

Wizara ya Afya imepokea paketi 2,952 sawa na pedi 29,520 ikiwa ni ishara ya kuzindua rasmi Kampeni ya kuchangia pedi kwa wanafunzi ambazo zitagawiwa kwa wasichana waliopokatika shule za msingi na sekondari nchini.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Wizara ya Afya, Prof. Pascal Ruggajo wakati alipomwakilisha Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel wakati akipokea pedi zilizotolewa na Kampuni ya Mawasiliano ya Simu Halotel.

“Pedi hizi ambazo tumezipokea zitasambazwa kwenye shule za Mkoa wa Dodoma kwa kuanzia na pedi zitaendelea kugawiwa kwa wasichana waliopo shuleni kadri zinavyo patikana”, ameeleza Prof. Ruggajo

Prof. Ruggajo amesema lengo la Kampeni hiyo ni kuchangisha paketi za pedi milioni 5 ambazo zitasambazwa kwenye shule ili kuhakikisha mtoto wakike anapata hedhi salama

Vile vile ametoa wito kwa wadau mbalimbali kujitokeza katika kampeni ya kuchangia pedi kwa wanafunzi ambazo zitagawiwa kwa wasichana waliopo katika shule za msingi na sekondari nchini ili kutatua changamoto ya upungufu wa pedi salama kwa matumizi ya wasichana na wanawake.

Amesisitiza kuwa elimu inahitajika zaidi kwa jamii ili kuona suala hilo ni Baraka na sio laana au mikosi kwani suala la hedhi limezungukwa na usiri mkubwa kiasi kwamba jamii inakosa fursa ya kujadili kwa uwazi namna ya kuliboresha kuanzia ngazi ya kaya hadi kwenye taasisi hivyo kuna ulazima wa jamii kwendelea kupatiwa elimu juu ya hedhi.

Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Jukwaa la Hedhi Salama imekuwa ikichukua hatua za kukabiliana na changamoto hizo ikiwa ni kuanzishwa kwa kampeni ya kuchangia pedi kwa wanafunzi yenye kauli mbiu ya Pedi Yangu Afya Yangu.