KAMATI YA PAC YAIPONGEZA WIZARA YA AFYA KWA KUBORESHA SEKTA YA AFYA
Posted on: March 26th, 2025
Na WAF - Moshi, Kilimanjaro
Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Mhe. Japhet Hasunga ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Kanda (KCMC) kwa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa jengo la huduma za tiba mionzi kwa matibabu ya wagonjwa wa saratani uliofunguliwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mhe. Hasunga ametoa pongezi hizo leo baada ya Kamati ya Bunge ya PAC kufanya ziara ya ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa jengo la huduma za tiba mionzi kwa matibabu ya wagonjwa wa saratani katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda (KCMC) na kupokea taarifa ya ujenzi unaotarajiwa kukamilika Aprili 30, 2025.
"Kazi ya kamati yetu ni kuangalia thamani ya fedha, kuishauri na kuisimamia Serikali, lakini niseme kwa mara ya kwanza tumeona jengo ambalo halina ghorofa lakini lina kuta nene, kwakweli niwapongeze tumeona majengo yanaonekana na fedha za Serikali zimetumika vizuri," amesema Mhe. Hasunga.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imetenga Shilingi Bilioni 1 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba pamoja na mahitaji mengine ili kukamilisha mradi huo wa ujenzi wa jengo la huduma za tiba mionzi kwa matibabu ya wagonjwa wa Saratani.
Vilevile, wakati akijibu swali la Mhe. Ester Matiko (MB) ambaye alitaka kujua kama huduma za kansa zimeanza kutolewa katika hospitali ya Bugando, Katibu Mkuu Dkt. Shekalaghe amesema zaidi ya miaka miwili (2) sasa huduma hizo zinaendelea kutolewa na Serikali inaendelea kotoa fedha za ujenzi pamoja na ununuzi wa vifaa tiba.
Awali wakati akiwasilisha taarifa ya mradi, Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda (KCMC) Prof. Gileard Masenga amesema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuboresha huduma za mionzi kwa wagonjwa wa saratani na kuwafanya wananchi wa mikoa ya Kaskazini kupata huduma bora za afya kwa wakati.