JAMII YATAKIWA KUACHA MAZOEA NATUMIZI YA DAWA ZA KIENYEJI KUTIBU MASIKIO YA WATOTO
Posted on: March 4th, 2026Na WAF-Mtwara
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Donald Wilson Msengi ametoa wito kwa jamii na wazazi wote nchini kuacha tabia ya kutumia dawa za kienyeji kutibu masikio ya watoto na badala yake wawe mstari wa mbele katika kuwaibua watoto wenye changamoto za masikio na usikivu ili waweze kupata huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Ametoa wito huo leo Machi 03, 2026 akiwa mgeni rasmi katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Usikivu Duniani ambayo Kitaifa yamefanyika Mkoani Mtwara katika Viwanja vya Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini yakiongozwa na kauli mbiu isemayo "Kutoka Jamii Hadi Darasani: Huduma ya Usikivu kwa Watoto Wote".
"Kila mtoto katika Taifa letu ana haki ya kusikia, kusikilizwa na kustawi kwani Kauli mbiu hii inasisitiza vipaumbele viwili muhimu kama vile kuzuia upotevu wa usikivu wa watoto unaoweza kuepukika au kuzuilika pamoja na kuhakikisha utambuzi wa mapema kwani zaidi ya 60% ya upotevu wa kusikia utotoni unaweza kuzuilika” alisisitiza Kanali Msengi.
Aidha amewahimiza wazazi kutafuta usaidizi wa kitaalamu katika vituo vya kutolea huduma za Afya pindi waonapo dalili za awali za kutokwa na maji maji au pale unapogundua mtoto ana usikivu hafifu kwani wazazi ndio watu wa kwanza kugundua mapema kuhusu maradhi ya masikio kwa mtoto hivyo waendelee kuwa karibu na watoto wao ili waweze kufuatilia ukuaji wao.
Sambamba na hilo, amewaasa wananchi kuacha imani potofu juu ya watu wenye matatizo ya usikivu kama vile uziwi unatokana na kurogwa, hautibiki, wenye changamoto hizo kutokuwa na akili hali ambayo inasababisha unyanyapaa katika jamii na kusababisha watoto kutoongea vizuri, ufaulu hafifu shuleni, kukosa kazi na kupata sonona kwa watu wazima.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Wizara ya Afya Dkt. Mwinyikondo Juma Amiri amewataka wananchi kuacha tabia ya kutumia vifaa vya kuongeza usikivu visivyozingatia ubora (earphones) na kupunguza kukaa sehemu zenye kelele nyingi ili kuendelea kulinda afya za masikio yao.