Customer Feedback Centre

Ministry of Health

INDIA KUSHIRIKIANA NA TANZANIA KATIKA UPATIKANAJI WA DAWA ZA BEI NAFUU

Posted on: July 25th, 2023

Na Mwandishi wetu, New Delhi, India.

Serikali ya India na Tanzania zimekubaliana kushirikiana katika upatikanaji wa dawa za gharama nafuu ili kuwezesha wananchi kumudu na kupata dawa hizo kwa gharama nafuu zaidi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu mara baada ya kukutana na kufanya kikao na Waziri wa Afya na Ustawi wa Familia wa India Mhe. Mansukh Mandaviya Jijini New Delhi India.

Katika kikao chao kilicholenga kujadili masuala mbalimbali ya uboreshaji wa Sekta ya Afya Waziri Ummy Mwalimu amesema kuwa suala la upatikanaji wa dawa na vifaa tiba vyenye ubora ni agenda muhimu kwenye ziara yake ambapo Viongozi hao wamejadili kwa kina fursa za uwekezaji nchini Tanzania kwenye Sekta ya Afya kwa ajili ya kuzalisha bidhaa za dawa ndani ya Tanzania hasa kwa kuwa asilimia 60 ya dawa na bidhaa za afya nchini Tanzania zinanunuliwa kutoka India, huku pia soko la dawa linagusa hadi nchi za Ukanda wa Jumuiya ya Afika Mashariki na Nchi za SADC, unafuu wa bei za dawa utasaidia kufikia watu wengi zaidi na hivyo kuwawezesha kupata tiba.

“Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano zaidi katika maeneo mbalimbali na Serikali na Wadau wa Sekta ya Afya kutoka India kwenye utoaji wa huduma za ubingwa bobezi kufuatia uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya Afya ambapo tumeshuhudia kuanza kutolewa kwa huduma za kibingwa ikiwemo upandikizaji wa Uloto (Bone marrow transplant), Upandikizaji Figo (Kidney transplant), upandikizaji wa vifaa vya usikivu ( Cochlea Implants), upasuaji wa moyo na mishipa ya fahamu” amesema Waziri Ummy.

Kwa upande wake Waziri Mansukh Mandaviya ameshukuru kutembelewa na Waziri Ummy Mwalimu na kuahidi kuimarisha ushirikiano katika kuboresha Sekta ya Afya kuanzia kwenye uzalishaji, upatikanaji wa dawa bora kwa bei nafuu kwa ajili ya manufaa ya nchi zote mbili.