Customer Feedback Centre

Ministry of Health

HUDUMA ZA FIGO ZAIMARIKA NCHINI- DKT. MAGEMBE

Posted on: August 16th, 2025

Na WAF, Dar es Salaam.

Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe ameeleza kuwa huduma za figo nchini zimeimarika, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa upandikizaji wa figo na kuwezesha wagonjwa 157 kuhudumiwa, ongezeko la vituo vya kusafisha damu kufikia 73 nchi nzima vyenye mashine 749 zinazohudumia zaidi ya wagonjwa 3,300.

Dkt. Magembe ameyasema hayo Agosti 15, 2025 wakati akifungua Mkutano wa 10 wa Kisayansi wa Chama cha Madaktari wa Magonjwa ya Figo Tanzania (NESOT) unaofanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 14 Agosti, 2025 jijini Dar es Salaam.

Dkt. Magembe amesema Wizara ya Afya imeahidi kuendelea kushirikiana na NESOT katika mafunzo, kuboresha huduma na kuiweka Tanzania kama kitovu cha upandikizaji figo na utalii wa tiba katika ukanda wa Afrika Mashariki na SADC. Dkt. Magembe pia amewapongeza NESOT kwa ushindi ulioiwezesha Tanzania kuchaguliwa kuandaa Mkutano wa Chama cha Madaktari bobezi wa Figo Afrika (AFRAN 2027), ambao utawaleta nchini Tanzania wataalamu wa magonjwa ya figo kutoka bara la Afrika, akiahidi Wizara kutoa kipaumbele katika kuhakikisha mkutano husika unakuwa wa mafanikio makubwa na kuitangaza zaidi Tanzania Kimataifa.

Pia Dkt. Magembe aliwaonyesha washiriki wa mkutano huo namna Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ilivyowezesha mageuzi makubwa katika sekta ya afya nchini. Aidha, Dkt. Magembe ameupongeza uongozi wa NESOT kwa juhudi zake tangu 2012 katika kuandaa mikutano ya kisayansi, kuboresha miongozo ya tiba na kuhamasisha kinga na utambuzi wa mapema wa magonjwa ya figo.

Mkutano huo umehudhuriwa na wataalamu wapatao 200 kutoka ndani na nje ya nchi wakiwemo washiriki kutoka Afrika kusini, Kenya, Tunisia na India.

Mkutano huo pia umehudhuriwa na Mashujaa “Champions” wa Figo wanne (4) waliopandikizwa figo nchini Tanzania.