Customer Feedback Centre

Ministry of Health

HUDUMA BORA ZA KIAFYA ZITATOLEWA KWA WAFANYAKAZI WA MRADI WA BOMBA LA MAFUTA GHAFI

Posted on: September 8th, 2023

Na. WAF - Dodoma


Serikali kupitia Wizara ya Afya imewahakikishia huduma bora za Kiasfya kwa wafanya kazi wa mradi wa Bomba la mafuta Ghafi la Afrika Mashariki linalotoka nchini Uganda kuja Tanzania pamoja na wananchi watakaopitiwa na mradi huo.


Hayo yamesemwa leo na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe kwenye kikao kati ya Wizara ya Afya, Idara ya Magonjwa ya dharura na Milipuko pamoja na Shirika la East Africa Cooperation Petroleum Pipeline (EACOP) kilichofanyika kwenye ofisi za Wizara hiyo Jijini Dodoma. 


“Tunawahakikishia huduma bora kwa wafanyakazi wa mradi huu, pamoja na wananchi wanaoishi pembezoni mwa mradi huu utakapopita usalama wa Afya zao, pamoja na kupatikana kwa mahitaji yote ya Kiafya yatakayohitajika ili kuhakikisha mradi huo unatekelezeka”. Amesema Dkt. Magembe


Amesema, Mradi huo ni ushirikiano baina ya nchi ya Uganda na nchi ya Tanzania ambao unahusika na kusafirisha mafuta kutoka Hoima nchini Uganda kwenda kwenye Bandari ya Tanga nchini Tanzania.


Aidha, Dkt. Magembe ameendelea kusema kuwa uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye eneo la miundombinu, vifaa tiba, pamoja na mafunzo kwa wataalamu. 


Vile vile amesema, kwa kiasi kikubwa Uwekezaji huo utasaidi kuboresha eneo la huduma bora kwa wananchi hasa kwenye eneo la magonjwa ya Dharura kwa wananchi pamoja na wafanyakazi wa mradi.


Mwisho, Dkt. Magembe amewahimiza wataalam wa Shirika hilo la EACOP kuendelee kuwaamini na kuwatumia wataalam wa Afya wenye utayari hasa kwenye eneo la magonjwa ya dharura kwenye mifumo ya huduma za dharura nchini Tanzania.