Customer Feedback Centre

Ministry of Health

HOSPITALI ZA INDIA NA TANZANIA KUENDELEZA USHIRIKIANO KATIKA HUDUMA ZA MATIBABU YA KIBINGWA

Posted on: July 26th, 2023

Waziri wa Afya Mhe Ummy Mwalimu ametoa wito kwa uongozi wa Hospitali za BLK-Max na MAX-Saket kuendelea kushirikiana na Tanzania katika utoaji wa huduma za matibabu ya kibingwa bobezi nchini Tanzania.

Waziri Ummy Mwalimu ametoa wito huo leo Julai 26, 2023 wakati akiendelea na ziara yake nchini India, ambapo ametembelea Hospitali za BLK - MAX Speciality Hospitali na MAX-Saket zilizopo mjini New Delhi na kueleza nia ya kuendeleza ushirikiano kwenye matibabu ya ubingwa bobezi kwenye magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, ini, figo, saratani, ubongo na mishipa ya fahamu.

“Naishukuru Hospitali za BLK-MAX Speciality na MAX-Saket kwa kuwajengea uwezo wataalam kutoka Tanzania taaluma ya kuanzisha huduma za kupandikiza figo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili mwaka 2017, huduma huduma za upasuaji mkubwa wa moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na pia kutoa mafunzo kazini kwa wataalam wa Mifupa na mishipa ya fahamu katika Taasisi ya Mifupa MOI” amesema Waziri Ummy.

Hata hivyo, ametumia fursa ya ziara hiyo kuwajulia hali wagonjwa mbalimbali kutoka Tanzania wanaopata huduma za matibabu katika Hospitali ya BLK - MAX ya mjini New Delhi, India.

Waziri Ummy amewaalika Uongozi wa BLK-Max na MAX-Saket kufungua Matawi ya Hospitali zao nchini Tanzania ili warahisishe utoaji wa huduma kwa wagonjwa wengi zaidi kwani uwekezaji huo utawapunguzia gharama za safari na muda kwa Watanzania na wananchi wengi wa Afrika Mashariki.

Hospitali hizo kubwa za kisasa zinatoa huduma mbalimbali za kawaida na za ubingwa bobezi ambapo wana madaktari bingwa na bobezi zaidi ya 4800 katika fani mbalimbali na zinauwezo wa kuhudumia wagonjwa zaidi ya milioni 3.5 kwa mwaka kutoka katika nchi zaidi ya 135.