Customer Feedback Centre

Ministry of Health

HOSPITALI YA APOLLO INDIA KUWEKEZA TANZANIA

Posted on: July 28th, 2023

Uongozi wa Hospitali ya Apollo umeahidi kuja Tanzania na kuwekeza katika Sekta ya Afya kwa kufungua Hospitali itakayokuwa imejikita kwenye utoaji wa huduma za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu mara baada ya kutembelea Hospitali hiyo iliyopo Jijini New Delhi India na kufanya kikao na uongozi wa Hospitali hiyo Mwenyekiti na Mwanzilishi wa Hosoitali Dkt. Prathap Chandra Raddy.

“Hospitali hii kubwa ya Apollo imekuwa na ushirikiano na Tanzania kwa kipindi kirefu sasa hususani katika kuwahudumia wagonjwa mbalimbali wanaopewa rufaa za matibabu ya kibingwa na ubobezi wa juu pamoja na magonjwa ambayo yanahitaji matibabu kwa kutumia teknolojia ya kisasa zaidi pamoja na kuendelea na programu ya kuwaongezea ujuzi wataalamu wa Sekta ya Afya katika maeneo ya ubingwa na ubobezi” Amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Waziri Ummy amesema kuwa kupitia mazungumzo yake na uongozi wa Hospitali hiyo chini ya Dkt. Prathap Chandra Raddy amekubali ombi la kufanya uwekezaji wa Hospitali kubwa itakayotoa huduma za kisasa kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

“Uwekezaji huu utakuwa umefanyika kwa wakati sahihi na utasidia sana katika kuwapunguzia gharama za matibabu wagonjwa wengi wanaohitaji matibabu ya kibingwa nje ya nchi. Kwa kuzingatia uhitaji huo, uwekezaji wa Taasisi ya Apollo utajikita katika Huduma za kibingwa ikiwemo upasuaji za kupandikiza Figo, Upandikizaji wa Ini, Upandikizaji wa Uloto, upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu, upasuaji mkubwa wa moyo na mishipa ya damu, ini, Figo, Saratani, Ubongo na Mishipa ya Fahamu” amesema Waziri Ummy.