Customer Feedback Centre

Ministry of Health

HOSPITALI SINGIDA YAPOKEA MASHINE YA KISASA KUTIBU MAGONJWA YA PUA, KOO NA MASIKIO KWA 80%

Posted on: March 20th, 2025

Na WAF, Singida

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida imepokea mashine ya kisasa kwa ajili ya matibabu ya magonjwa ya Pua, Koo na Masikio (ENT) yenye thamani ya Shilingi Milioni 360, iliyotolewa na shirika lisilo la kiserikali la “Doctors for The Destitutes Foundation” (D4D).

Mashine hiyo imepokelewa leo Machi 19, 2025 ikiwa ni matokeo ya ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na shirika hilo katika kuboresha sekta ya afya nchini.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Singida ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Victorina Ludovick, amesema kupatikana kwa mashine hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuboresha huduma za afya nchini.

“Serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha hospitali zetu zinakuwa na vifaa tiba vya kisasa kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa wananchi,” amesema Dkt. Ludovick na kuongeza kuwa,

“Jukumu lililo mbele yetu ni kuitunza kwa kuifanyia matengenezo pale inapohitajika ili idumu kwa muda mrefu”, amesisitiza Dkt. Ludovick.

Kwa upande wake mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, Mkunga Bingwa, Bi. Hilda Mushi, amewashukuru wadau wa D4D kwa kuiunga mkono Serikali kwa msaada na kusema lengo la Serikali ni kuendelea kuimarisha huduma kwa ushirikiano na wadau wa maendeleo huku Serikali ikijizatiti kuongeza wataalam bingwa.

“Mashine hii itakuwa msaada mkubwa kwenu, itasaidia kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda hospitali za juu kama Benjamin Mkapa, KCMC ama Bugando na Muhimbili,” amesema Bi. Mushi.

Naye Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali hiyo Bw. Baraka Muhembano, amesema upatikanaji wa mashine hiyo unaenda sambamba na jitihada za kuboresha huduma za afya katika ngazi ya mkoa.