HAKUNA CHANGAMOTO YA USAMBAZAJI WA DAWA NCHINI
Posted on: November 1st, 2024Na WAF-Dodoma
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amesema kwa sasa hakuna changamoto ya usambazaji wa dawa, vifaa, na vifaa tiba nchini, hali ambayo imewezesha vifaa hivyo kufika kwa wakati kwenye maeneo husika kutokana na uwekezaji uliofanywa na Serikali ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya na kuimarisha mfumo mzima wa usambazaji wa dawa na vifaa tiba.
Hayo yamebainishwa bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mhe. Nancy Hassan Nyalusi Mbunge wa viti maalumu ambaye alitaka kujua ni lini Serikali itapeleka mtaji Bohari ya Dawa (MSD).
Aidha Dkt. Mollel amesema Serikali imekwishatoa fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 100 kama mtaji kwa MSD kati ya Shilingi Bilioni 561.5 iliyopangwa kutolewa hadi kufikia Oktoba 2024.
Dkt. Mollel amesema fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 100 ni mtaji kwa MSD na kwamba kila mwezi inapokea kiasi cha Shilingi Bilioni 16.7 kwa ajili ya ununuzi wa dawa huku Bilioni 100 zikiwa zimeelekezwa na MSD kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa viwanda.
Dkt. Mollel ameendelea kusema kuwa Serikali itaendelea kutoa fedha hizi kwa awamu kulingana na upatikanaji wake.