Customer Feedback Centre

Ministry of Health

GLOBAL HEALTH FOUNDATION YA NCHINI INDIA KUSHIRIKIANA NA TANZANIA KATIKA MAFUNZO YA WATAALAM NA UTOAJI WA HUDUMA ZA AFYA

Posted on: July 30th, 2023

Taasisi ya Global Health Foundation ya nchini India imejipanga kushirikiana na Tanzania katika mafunzo ya wataalam na utoaji wa huduma za afya kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu Julai 30, 2023 alipotembelea Taasisi hiyo iliyopo Hyderabad nchini India.

“Naupongeza Uongozi wa Taasisi hii kwa ubunifu na uvumbuzi wa teknolojia mbalimbali ambazo zinachangia mapinduzi makubwa ya utoaji wa huduma za afya duniani kote ikiwemo Tanzania. Naikaribisha Taasisi hii ili ishirikiane na Serikali kwa kuingia makubaliano ya ushirikiano kwenye eneo la Mafunzo kwa Wataalam, Sayansi, Huduma za Afya na Tehama” amesema Waziri Ummy.

Kwa upande wake mwanzilishi wa Taasisi hiyo, Dkt. Ravindrapath Kancharla alieleza kuwa, Taasisi yake pamoja na kuendesha huduma za utoaji wa Afya, sasa wameamua kuwekeza zaidi kwenye ugunduzi na matumizi ya Tehama katika kuleta mapinduzi zaidi kwenye sekta ya Afya.

Amesema kuwa Global Health Foundation imeanzisha Chuo Kikuu cha Afya, Sayansi na Teknolojia ( Global Health - Tech Life Sciences University and Innovation Hub) ili wajikite zaidi kwenye kutoa mafunzo, utafiti na ugunduzi wa teknolojia mbalimbali kusaidia utoaji wa huduma bora za Afya.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo tarehe 30.07.23 amemaliza ziara yake ya kikazi nchini India, kwa kutembelea na kufanya mazungumzo na uongozi wa Taasisi ya Global Health Foundation ya mjini Hyderabad, India. Taasisi hii imeanzisha Chuo Kikuu cha Afya, Sayansi na Teknolojia ( Global Health - Tech Life Sciences University and Innovation Hub) ili wajikite zaidi kwenye kutoa mafunzo, utafiti na ugunduzi wa teknolojia mbalimbali kusaidia utoaji wa huduma bora za Afya.

“Tumegundua teknolojia inayosaidia kujua kama mgonjwa amefanyiwa huduma za dialysis ipasavyo, tumegundua pia kifaa kinachowasaidia watoto wenye usonji (Autism) kujifunza kuongea ambapo kifaa hicho kina uwezo wa kutumia lugha mbalimbali ulimwenguni ikiwemo kiswahili” amesema Dkt. Ravindrapath Kancharla.