Customer Feedback Centre

Ministry of Health

ENDELEENI KUMSAIDIA DKT. SAMIA KULINDA AFYA ZA WATANZANIA- MHE. NYONGO.

Posted on: September 11th, 2023

Na Waf - DSM. 


Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI Mhe. Stanslaus Nyongo ametoa wito kwa mamlaka ya dawa na vifaa tiba nchini (TMDA) kuendeleza ufanisi walionao katika kuangalia ubora na usalama wa dawa na vifaa tiba ili kuzilinda afya za Watanzania.


Mhe. Nyongo ametoa wito huo leo Septemba 11, 2023 wakati ziara ya kamati ya kudumu ya Bunge ya afya na masuala ya UKIMWI ilipotembelea Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba ili kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Mamlaka hiyo katika kuzilinda Afya za Watanzania. 


"Sisi kama Wabunge, wawakilishi wa wananchi tunawategemea sana kwa usalama wa dawa zetu ambazo zinaenda kwa mwananchi ambae ndio mlaji wa dawa hizo". amesema Nyongo


" TMDA mnamlinda afya za watanzania, endeleeni na moyo huo, mnamsaidia Mhe. Rais katika kulinda jamii ya Watanzania kupitia usalama wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi. " Amesema. 


Baada ya ziara ya kukagua shughuli mbalimbali katika Mamlaka hiyo, Mhe. Nyongo ametoa rai kwa wananchi kuwa na imani na Mamlaka hiyo kwani inafanya kazi kubwa yenye ufanisi na inatambulika na Shirika la Afya Duniani kwa kupewa ithibati daraja la nne.


Aidha, Mhe. Nyongo amewataka wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa vyombo husika ikiwemo TMDA kupitia *152*00# na kubofya namba 2 endapo watakutana na dawa ambazo sio salama na kuleta madhara katika jamii ili changamoto hiyo ishughulikiwe kwa haraka.


Sambamba na hilo, amewataka Serikali kupitia Wizara ya Afya kukaa na Wizara ya viwanda kuona namna ya kurejesha usalama wa chakula chini ya Wizara ya Afya kupitia Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba kwani ufanisi na ubora wa TMDA unaotambulika katika Shirika la afya Duniani utasaidia kwa kiwango kikubwa juu ya usalama wa chakula nchini. 


Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amewapongeza Watumishi wa TMDA kwa jitihada kubwa katika utendaji unaosaidia usalama wa wananchi kupitia Dawa, vifaa tiba na vitendanishi. 


Ameongeza kuwa, Wizara ya Afya inaendelea na makubaliano na Wizara ya viwanda ili kuona namna gani ya kurudisha Chakula chini ya Mamlaka ya dawa na vifaa tiba kulingana na utaratibu wa Shirika la Afya Duniani. 


Mwisho.