BENJAMIN MKAPA YAWEKA VIPAUMBELE KWENYE UBORA, USALAMA WA MGONJWA
Posted on: September 17th, 2025
Na WAF - DODOMA
Hospitali ya Benjamin Mkapa imeendelea kuweka kipaumbele katika usalama wa mgonjwa kwa kuhakikisha huduma zinazotolewa zinazingatia viwango vya ubora, usalama na mahitaji ya mgonjwa.
Hayo yamebainishwa Septemba 17, 2025 na Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Dkt. Henry Humba katika Maadhimisho ya Siku ya Usalama wa Mgonjwa Duniani, katika Hospitali ya Benjamini Mkapa, jijini Dodoma.
Dkt. Humba amesema hospitali yake inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ili kuhakikisha jamii inanufaika na huduma salama na zenye ubora.
Aidha Dkt. Humba ameeleza kuwa ni matarajio ya BMH kuona wazazi, hususan baba wa watoto, wakishiriki kikamilifu katika huduma za uzazi.
Aidha Dkt. Humba amesisitiza kuwa ili wazazi washiriki kwa ufanisi, inahitajika elimu ya kutosha pamoja na mabadiliko ya mtazamo wa kijamii.
Kwa upande wake Dkt. Emmy Mbilinyi, Daktari Bingwa wa Watoto amesema wakati wa kutoa huduma, madaktari na watoa huduma wa afya wanapaswa kushirikiana kwa karibu na wazazi.
“Hatua hii inaleta mazingira salama ya utoaji huduma ambapo kila mzazi anajihisi kuwa sehemu ya mchakato wa kulea na kutunza mtoto,” amesema Dkt. Mbilinyi.
Dkt. Mbilinyi ametoa wito kwa wauguzi na watoa huduma wengine wa afya kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu na msaada kwa wakina mama.
Sambamba na hayo, wakina mama wametakiwa kuhakikisha kuwa wanapokutana na changamoto au matatizo ya kiafya, wanakwenda mara moja katika vituo vya kutolea huduma kwani hatua ya kuchelewa kupata matibabu inaweza kuongeza hatari kwa mama na mtoto.
Ameeleza kuwa pamoja na huduma jumuishi zinazotolewa kwa watoto, BMH pia inatoa huduma za kibingwa na bobezi kwa watoto, hatua ambayo imeifanya hospitali hiyo kuwa kimbilio la afya bora kwa wananchi kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania.