ALIYETESEKA MIAKA SABA KWA UVIMBE WA KIZAZI, ANUFAIKA NA HUDUMA YA UPASUAJI
Posted on: May 16th, 2024
WAF - Rukwa
Jopo la Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia Suluhu Hassan waliokita kambi katika Hospitali za Halmashauri na wilaya za mkoa wa Rukwa, wamefanikiwa kufanya upasuaji kwa mwanamke (33) mkazi wa Manispaa ya Sumbawanga aliyeteseka na uvimbe katika kizazi (multiple mayoma) kwa miaka 7.
Akizungumza baada ya Upasuaji leo Mei 16, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya wanawake na Uzazi, Dkt. Emmanuel Imani Ngadaya amewaasa wananchi kufika katika Hospitali na kupata vipimo na ushauri wa kitaalamu badala ya kwenda kwa waganga wa kienyeji wakiamini wamerogwa, kwa matatizo yanayohitaji upasuaji.
"Tumegundua mnufaika wa upasuaji huu amesumbuka kwa miaka saba ametumia dawa nyingi na kuna kipindi anaonekana alienda kwa waganga wa kienyeji kupata dawa za kienyeji ambazo tuliziondoa.
"alikuwa anapitia maumivu makali akiwa na vimbe ndogondogo zaidi ya saba, na alipofika kliniki alikuwa akilia, hana fedha amehangaika, hivyo tumemfanyia upasuaji ambao utaondoa kadhia ambazo angeendelea kuzipata kwa muda mrefu, ikiwemo saratani ya kizazi hapo baadae.
Mwananchi huyo amefanyiwa upasuaji kwa msamaha (exemption) ambapo amechangia kiasi cha elfu 30 kwa huduma ambayo angehitaji kulipa zaidi ya laki 8 na kusafiri umbali mrefu kupata huda hizo za kibingwa.
Madaktari hao wanaendelea kutoa huduma za kibingwa katika Hospitali za Halmashauri za wilaya ndani ya Mkoa wa Rukwa, ikitarajiwa Mpango huo Kabambe wa Madaktari Bingwa kufikia tamati hapo kesho, Ijumaa Mei 17, kwa mkoa wa Rukwa, huku kwa nchi nzima ikitarajiwa kufikia ukomo Juni 28, mwaka huu.
Lengo la Mpango Kabambe wa Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia, ni kusogeza huduma za kibingwa na Bobezi karibu na wananchi, pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu waliopo katika Ngazi ya Afya ya Msingi.