Customer Feedback Centre

Ministry of Health

AJENDA YA KUTOKOMEZA MALARIA, RAIS SAMIA AMEONESHA IMANI - DKT. KIKWETE

Posted on: April 13th, 2024


Na WAF, Arusha


Rais Mstaafu wa Awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameonesha imani kwa viongozi aliowateua kusimamia baraza la kuongoza mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria hivyo hawana budi kuja na afua zitakazo iwezesha nchi kufikia azma yake ya kutokomeza Malaria.


Dkt. Kikwete ambaye ni Mjumbe wa kamati ya Dunia wa amesema hayo Aprili 13, 2024 jijini Arusha wakati wa ziara yake kwenye kiwanda cha kuzalisha vyandarua kilichopo mkoani humo cha A to Z.


“Miongoni mwa wajumbe tulioteuliwa na Rais ni watu ambao tumeshafanya mambo makubwa katika jamii, hivyo imani ya Mhe. Rais ni kubwa kwetu tunasema, alitupa imani, hivyo ni vyema tukamlipa imani, ni rai yangu tuoneshe fadhila kwa kushirikiana na jamii kuja na afua zitakazo wezesha kufikia azma". Amesema Dkt. Kikwete.


Aidha, Dkt. Kikwete amesema kuanzia sasa nchi ni lazima ianze kuwaza kwenye kuzuia na kutokomeza kabisa Malaria ikiwemo kutekeleza afua kama vile kuua viluilui vya mazalia ya mbu ambayo ni chanzo kikuu cha ugonjwa huo.


Ameongeza kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi 11 zilizo kwenye maambukizi makubwa ya Malaria, huku bara la Afrika likiwa linaathiriwa na malaria kwa asilimia 93 na asilimia saba ndio nchi zingine za dunia.


“Takwimu hizi sio nzuri kabisa, hivyo lazima tuje na majibu ya kisayansi kwa masuala haya ya kisayansi, katu tusilete siasa, wenzetu A to Z hapa Arusha wameonesha mfano na nilipokuwa na wajumbe wenzangu wa Dunia wakanituma nije nitembelee kiwanda hiki na kwakweli nimejionea kazi wanayofanya ni njema". Amesema Dkt. Kikwete.


Akitoa salaam za Wizara Dkt. Catherine Joachim amesema zipo sababu kadhaa zinazo changia kufanya usugu kwenye mwili wa mtu hasa matumizi yasiyo sahihi ya dawa.


“Kuna baadhi ya watu akiugua bila hata kupima anakwenda kununua dawa na kumeza lakini wakati mwingine watu kutokumaliza dozi wanazo andikiwa na wataalam, hii imekuwa ni changamoto hivyo tunawashauri watu pindi asikiapo dalili za ugonjwa ni vema akawaona wataalam akapima ndio ameze dawa” amesema Dkt. Catherine.


Pia amemshukuru Mwenyekiti wa Kamati ya kutokomeza Malaria nchini kwa jitihada anazo chukua kama mtanzania kuhakikisha mipango ya Serikali kutokomeza Malaria ifikapo 2030 inatimia.


“Kwa Nchi za Afrika Mauritius, mwaka 1973 walifanikiwa kutokomeza Malaria, Cape Vede mwaka 1918 na Algeria 1919 walifanikiwa kuondokana na Malaria, hivyo na sisi tukisimama kwa sauti moja tutafanikiwa”. Amesema Dkt. Catherine

 

Kando ya Mkutano huo, wajumbe wa baraza hilo, Mufti Mkuu wa Tanzania Alhaj Abubakar Zuber na rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania Mhashamu Baba Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga, wamesema, watatumia majukwaa ya nyumba za ibada kuwaelimisha waumini umuhimu watokomeza malaria.


MWISHO