AFUA KUPUNGUZA VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI ZAING'ARISHA TANZANIA KIMATAIFA
Posted on: December 7th, 2024Na WAF, Dodoma
Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto kutoka Wizara ya Afya Dkt. Ahmad Makuwani amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuhakikisha kila hospitali ya wilaya nchini inaanzisha kitengo cha uangalizi maalumu wa watoto wachanga na watoto wenye uzito pungufu (NICU) ili kuendelea kupunguza vifo vya watoto.
Dkt. Makuwani amesema hayo Desemba 6, 2024 wakati wa kikao cha majumuisho ya ziara ya ugeni wa nchi 14 ukiongozwa na shirika la kudhibiti magonjwa Afrika (CDC Africa) wenye lengo la kujifunza utekelezaji wa afua zilizotekelezwa na Serikali ya Tanzania ili kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga.
Dkt. Makuwani amesema Serikali imejenga vyumba maalumu vya upasuaji (CEmONC) katika vituo vya Afya na kuanzisha vyumba vyenye vitanda vya kuwaangalia watoto wachanga na watoto wenye uzito upungufu na kuwapatia rufaa ya kwenda hospitali ya wilaya jirani pale inapohitajika huduma na uangalizi zaidi.
Katika hatua nyingine Dkt. Makuwani ameushukuru ugeni huo kwa kuchagua Tanzania kuwa sehemu sahihi ya kujifunza namna bora ilivyoweza kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga.
“Suala ya kupunguza vifo vya mama na watoto wachanga liko mikononi mwenu na msitegemee watu kutoka mataifa ya nje kuja kuwafanyia kazi hiyo, wanachoweza kufanya wao ni kutoa ufadhili ila nguvu na jitihada ziwe kwenu,” amesema Dkt. Makuwani.
Akizungumza kwa niaba ya ugeni huo mjumbe kutoka nchini Guinea Conakry, Dkt Anne Marie Soumah amesema wanaenda pamoja kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ambayo kwa kweli inaendelea kurekodi kesi hizo.
“Tunaweza kuokoa mwanamke na mtoto wake lakini kutokana na hali halisi wakati mwingine tunapoteza wanawake ilihali tunaweza kuwaokoa. Ni jambo la kuridhisha sana hasa kwa upande wangu ambapo ziara hii ilikuwa ni fursa ya kujitia moyo kwa mambo mengi mazuri ambayo Tanzania imelazimika kuyafikia na ambayo tunaweza kuyatekeleza katika nchi zetu mbalimbali,” amesema Bi. Soumah.