ACHANENI NA IMANI POTOFU JUU YA MATIBABU YA MACHO
Posted on: November 2nd, 2024
NA WAF – MBEYA
Wananchi wa Kyela wametakiwa kuachana na imani potofu kuhusu matibabu ya macho na badala yake watumie huduma za afya zinazotolewa na wataalamu wa afya.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Mhe. Josephine Manase, Novemba 02, 2024, wakati akifunga kambi ya matibabu ya macho, iliyofadhiliwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Helen Keller.
“Wilaya ya Kyela kuna tatizo kubwa la watu wenye ugonjwa wa mtoto wa jicho. Hivyo, zinapokuja fursa kama hizi za matibabu, wananchi wanapaswa kuachana na dhana potofu na kuzichangamkia kwa sababu zinatoa suluhisho la moja kwa moja kwa matatizo haya ya macho na kusaidia kuboresha afya ya jamii,” amesema Mhe. Manase.
Mhe. Manase amesema zaidi ya wagonjwa 400 wamefanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho kupitia kambi ya siku saba ya madaktari bingwa wa macho iliyofanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Kyela, Mkoani Mbeya.
“Ni muhimu kwa wazazi kuwaleta watoto wao wenye ugonjwa wa mtoto wa jicho kwa matibabu, badala ya kuwaficha,” amesema Mhe. Manase.
Aidha, Mhe. Manase ameishukuru Serikali na Shirika la Helen Keller kwa ushirikiano wao wa karibu katika kufanikisha kambi hii ya matibabu. Ushirikiano huu ni muhimu katika kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi na unaonyesha dhamira ya pamoja katika kuboresha afya ya macho wilayani Kyela.
Kwa upande wake, Meneja Mradi wa Shirika la Helen Keller, Bw. Athuman Tawakal, amesema kambi hii inatoa huduma za matibabu ya macho, ikilenga kutatua changamoto zinazohusiana na ugonjwa wa mtoto wa jicho, ambao umekuwa ukiathiri uwezo wa kuona wa watu wengi katika jamii.
Bw. Tawakal ameishukuru Serikali kwa ushirikiano mkubwa waliotoa kuanzia hatua za maandalizi ya kambi ya matibabu hadi kukamilika kwake.