Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WIZARA YA AFYA YAANZA USIMAMIZI SHIRIKISHI WA TIBA ASILI NA TIBA MBADALA MKOANI MOROGORO.

Posted on: November 25th, 2025

Na WAF, Morogoro

Wizara ya Afya kupitia Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala imeanza rasmi zoezi la usimamizi shirikishi mkoani Morogoro kwa lengo la kutoa elimu, kusajili na kutoa vyeti kwa waganga wa tiba asili na tiba mbadala.

Akizungumza wakati wa kikao na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Bi.Prisca Gallet Novemba 25, 2025, Msajili wa Baraza hilo, Bi. Lucy Mziray, amesema zoezi hilo linawalenga waganga wapya pamoja na wale waliokwishasajiliwa awali ili kuhuisha leseni zao zilizomaliza muda wake.

“Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala kuanzia wiki ya Novemba 24,2024 tupo mkoani Morogoro mpaka Disemba Mosi tukihamasisha, kuwafundisha na kuwakumbusha waganga mambo mbalimbali kuhusu majukumu yao pamoja na usajili wa papo kwa papo,” amesema Bi. Mziray.


Ameongeza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha huduma za tiba asili na tiba mbadala zinatolewa kwa kufuata miongozo ya Serikali, sambamba na kuhakikisha wataalam wote wanazingatia maadili na usalama wa wananchi.

“Tunawaomba waganga wote, pamoja na wamiliki wa vituo vya huduma za tiba mbadala, kujitokeza kwa wingi na kufika katika halmashauri zao kwa waratibu wa huduma hizo ili kusajili vituo na huduma zao, pamoja na kuhuisha sajili zilizokwisha muda. Kazi hii inafanyika Ulanga, Malinyi, Mlimba, Ifakara, na kuhitimishwa Morogoro Mjini,” amefafanua.

Kwa upande wake, Mratibu wa huduma za tiba asili na tiba mbadala kutoka wizara ya Afya Bw. Mussa Lipukuta amesema hatua hiyo itasaidia kuimarisha utoaji wa huduma za tiba asili na tiba mbadala ambazo zimeendelea kuwa chaguo muhimu kwa sehemu ya wananchi na zina mchango mkubwa katika kuchochea ustawi wa jamii.

Bw. Lipukuta ameongeza pia kuwa usimamizi huo shirikishi utaiwezesha Serikali kuwa na takwimu sahihi za watoa huduma, kusaidia kufuatilia viwango vya utoaji huduma, pamoja na kudhibiti vitendo vya kutoa huduma holela zisizofuata taratibu.