Wizara Ya Afya

TANZANIA BARA, ZANZIBAR ZAIMARISHA USHIRIKIANO WA UFUATILIAJI NA TATHMINI KATIKA SEKTA YA AFYA

Posted on: March 9th, 2026

Na Cletus Sanga, WAF - Dodoma

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimeendeleza ushirikiano wao katika sekta ya afya kupitia ziara ya kikazi iliyolenga kuimarisha ufuatiliaji na tathmini (Monitoring and Evaluation – M&E) wa programu za afya.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 09 Machi, 2026 na Mkurugenzi wa Idara ya Tathmini na Ufuatiliaji, Bw. Claude Kumalija katika kikao cha kubadilishana uzoefu Wizara ya afya na kitengo cha ufuatiliaji na tathmini na Wizara ya afya Zanzibar Kitengo cha ufuatiliaji na tathmini kilichofanyika jijini Dodoma.

Bw. Kumalija amesema kuwa Wizara ya Afya Zanzibar imefanya ziara ya siku tano katika Wizara ya Afya Tanzania Bara kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuimarisha utendaji kazi katika nyanja za ufuatiliaji na tathmini ya huduma na miradi ya afya.

Amesema katika ziara hiyo, timu ya wataalamu kutoka Zanzibar imepata fursa ya kujifunza kuhusu muundo wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini (DME), mifumo ya ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu za afya, pamoja na namna taarifa hizo zinavyotumika kufanya maamuzi ya kisera na kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.

Aidha, ameeleza kuwa mazungumzo kati ya pande hizo mbili yamejikita katika kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa programu za afya, kuboresha matumizi ya takwimu katika kupanga na kutathmini afua za afya, pamoja na kuendeleza mbinu bora za tathmini ya miradi na programu za sekta ya afya.

Bw. Kumalija ameongeza kuwa pande zote mbili zimekubaliana kuandaa Mpango wa Ushirikiano (Collaboration Plan) utakaoainisha maeneo ya kipaumbele, mgawanyo wa majukumu, mfumo wa utekelezaji pamoja na ratiba ya shughuli za pamoja katika kuimarisha ufuatiliaji na tathmini.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Wizara ya Afya Zanzibar, Bi. Khadija Rashid amesema kuwa ziara hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwa kuwapatia fursa ya kujifunza mbinu bora za ufuatiliaji wa miradi na programu za afya pamoja na matumizi sahihi ya takwimu katika kupanga na kutathmini huduma za afya.