KAMATI YA BUNGE YAPOKEA TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA AFYA NCHINI.
Posted on: March 10th, 2026Na Aisha Swahibu, WAF - Dodoma
Wizara ya Afya imeendelea na utekelezaji pamoja na usimamizi wa miradi ya maendeleo hususan miradi ya ujenzi wa miundombinu katika Hospitali ya Taifa, Kanda, Mikoa na Vyuo vya Afya ambayo iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Florence Samizi leo Machi 10, 2026 wakati akiwasilisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo iyotengewa fedha kwa mwaka wa fedha 2025/26 mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi.
Dkt. Samizi ameeleza kuwa katika kipindi cha Julai 2025 hadi Februari 2026, Wizara imesimamia na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya ujenzi 40 ambapo, kati ya miradi hiyo, miradi 27 inatekelezwa katika Hospitali za Rufaa za Mikoa, miradi 13 inatekelezwa katika ngazi ya Taifa, Hospitali Maalum na Hospitali za Kanda.
“Utekelezaji wa Miradi hiyo upo katika hatua mbalimbali ambapo Miradi saba imefikia zaidi ya asilimia 90, Miradi nane imefikia wastani wa asilimia 70, Mradi mmoja umefikia wastani wa asilimia 45, na Miradi 24 utekelezaji wake umefikia asilimia 13,” amesema Dkt. Samizi.
Amesema ukamilishaji wa miradi hiyo ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuhakikisha kila mtanzania anapata huduma za afya za kibingwa na ubingwa bobezi karibu na maeneo yao.