Wizara Ya Afya

MODULI ZA MAABARA TANZANIA KUWIANA NA ZA KIMATAIFA

Posted on: March 8th, 2026

Na Atley Kuni-WAF, Dar es Salaam

Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) chini ya mradi wa Pandemic Fund wanakamilisha moduli za kuwafundishia wataalamu wa maabara kwenye ngazi zote ili kuleta uwiano wa moduli za ndani na za kimataifa.

Hayo yamesemwa na Bi. Valentine Sanga Mratibu wa dawati la Afya moja kutoka Ofisi Waziri Mkuu, Bunge Sera, Uratibu na wenye Ulemavu wakati wa kikao kazi cha wataalam wa maabara Machi 9, 2026 jijini Dar es Salaam.

"Moja ya ya Malengo ya mradi wa Pandemic Fund ni kuhakikisha tunawajengea uwezo wataalam wa Maabara ili waweze kukabiliana na Magonjwa ya mlipuko mathalan Mabag na Ebola" amesema Bi. Sanga.

Kwa upande wake Bi. Ritha Massawe mratibu wa Pandemic Fund Maabara Wizara ya Afya, amesema kuwa, kupitia mradi huo utawezesha kuboresha shughuli za ulinzi na usalama wa Vimelea hatarishi kwa sekta zote ndani ya nchi.

"Baada ya kukamikika kwa maboresho ya hizi Moduli, zoezi litakalofuata ni kutolewa mafunzo nchi nzima kwa wataalam kwa njia mtambuka ikiwepo kwa Masafa ya marefu" amesema Bi. Ritha.

Naye mmoja ya washiriki wa zoezi hilo, Bi. Ashura Faraji Mtaalam wa Maabara kutoka Maabara ya Zanzibar (ZPHL), amesema maboresho ya Moduli yamekuja kwa muda muafaka kutokana na baadhi ya wataalam kutokuwa na uelewa mpana juu ya ulinzi na usalama wa vimelea hatarishi.

Hii inakuwa fursa ya kipekee ya kuwajengea uwezo ili kutimiza majukumu yao kwa weledi na maarifa zaidi.

Mradi wa Pandemic Fundi ni Mradi wa miaka mitatu unaosimamiwa na Shirika la Afya Duniani kwa ushirikiano na Wizara ya Afya na unatazamiwa kumaliza shughuli zake ifikapo Desemba, 2027.