Wizara Ya Afya

VITUO 36 KUTEKELEZA KITITA JUMUISHI CHA HUDUMA ZA AFYA YA MAMA NA MTOTO DAR ES SALAAM

Posted on: March 6th, 2026

Na Abduly Iddy, Dar es Salaam.

Serikali imeanzisha utekelezaji wa kitita jumuishi cha huduma za afya ya mama na mtoto chenye lengo la kuimarisha ubora wa huduma na kupunguza vifo vya mama na watoto wachanga nchini.

Akizungumza katika kikao cha utambulisho wa mpango huo kilichofanyika Machi 5, 2026 katika Mkoa wa Dar es Salaam, Katibu Tawala wa Mkoa huo Abdul Mhinte amesema mpango huo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuongeza kasi ya kupunguza vifo vya mama na watoto wachanga kwa kuboresha huduma katika vituo vya afya.

Amesema katika utekelezaji wa mpango huo, jumla ya vituo vya afya 36 vimechaguliwa katika Mkoa wa Dar es Salaam ili kuwa vituo vya mfano vitakavyoonyesha utekelezaji bora wa huduma za afya ya mama na mtoto.

Aidha, mpango huo pia unahusisha usambazaji wa vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na utoaji wa mafunzo na mafunzo elekezi kazini kwa watoa huduma ili kuhakikisha huduma zinazotolewa zinaendana na viwango vya kitaifa na kimataifa.

Kwa mujibu wa viongozi wa afya, kitita hicho kitazingatia maeneo manne muhimu ya huduma ambazo ni huduma za wajawazito kabla ya kujifungua, huduma wakati wa kujifungua, huduma za watoto wachanga pamoja na huduma za mama baada ya kujifungua.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha mama na mtoto wanapata huduma salama na bora kuanzia kipindi cha ujauzito hadi baada ya kujifungua.

Serikali kupitia Wizara ya Afya imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya afya ili kuhakikisha utekelezaji wa mpango huo unaleta matokeo chanya katika kuboresha afya ya mama na mtoto na kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika