Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAZIRI MKUU AFANYA ZIARA YA KUSHITUKIZA HOSPITALI YA MKOA WA DODOMA

Posted on: November 16th, 2025

Na WAF, Dodoma

Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba leo Novemba 15, 2025 amefanya ziara ya kushitukiza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na kuziagiza hospitali zote nchini kuhakikisha wajawazito wanapofika hospitali wanahudumiwa kwa haraka ili kuokoa maisha ya mama na mtoto.

Pia, ameiagiza Wizaya ya Afya, Bohari ya Dawa (MSD) na Hospitali zote nchini kuweka vipaumbele vya kuwa na dawa kulingana na mahitaji ya eneo husika.

“Haipendezi mwananchi kufika hospitali na kupatiwa vipimo vyote kisha anaambiwa dawa akanunue kwingine, kama duka binafsi linaweza kupata dawa hizo, inawezekanaje hospitali za Serikali hapati? Naagiza hospitali zote ziwe na dawa,” amesisitiza Waziri Mkuu.

Ametoa maagizo hayo wakati akizungumza na wananchi nje ya hospitali hiyo baada ya kutembelea wananchi waliofika hospitalini hapo kupata huduma mbalimbali za matibabu na kuwahakikishia wananchi kuendelea kuhudumiwa vizuri kwa kuwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha huduma za afya nchini vikiwemo vifaa tiba na dawa.

Aidha Waziri Mkuu ameziagiza hospitali zote nchini zihakikishe zinakuwa na vifaa vya usafi binafsi vya dharura vikiwemo ndoo na beseni katika wodi za wazazi ili viwasaidie akinamama wasiokuwa na vifaa hivyo.

“Ujauzito sio suala la dharura vifaa kama ndoo tunapaswa kuwa navyo katika hospitali zetu za Serikali, ” ameeleza Mhe. Dkt. Nchemba.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameziagiza hospitali zote nchini kuzingatia maelekezo ya kutumia mifumo sahihi ya malipo katika taratibu za kutoa huduma ili kuwezesha Serikali kuendelea kuhudumia wananchi.

Dkt. Nchemba ameeleza kuwa baadhi ya hospitali hupokea baadhi ya malipo ya huduma kwa njia ya mtandao na mengine kwa njia zisizo rasmi.