Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WANANCHI SONGWE WACHANGAMKIA FURSA YA MATIBABU YA UPASUAJI MTOTO WA JICHO

Posted on: September 17th, 2025

Na WAF - Songwe

Kambi maalumu ya upasuaji wa mtoto wa jicho inaendelea mkoani Songwe ikiwa ni siku ya nne (4) ambapo zaidi ya macho 400 yamefanyiwa upasuaji huku lengo likiwa ni kufikia macho 720 kwa siku sita (6) ili kutatua changamoto kwa wagonjwa hao kwakuwa mtoto wa jicho anatibika.

Afisa Mradi wa Shirika la Kimataifa la Helen Keller International Bw. Allen Lemilia amesema hayo leo Septemba 17, 2025 wakati kambi hiyo ya macho ikiendelea katika Hospitali ya Wilaya ya Vwawa, Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe inayotolewa na madaktari bigwa wa macho bila malipo.

"Kwa wastani wa kufanya upasuaji ni 120 kwa siku, tunategemea kufanya upasuaji wa macho 720 na leo ni siku ya nne kwenye matibabu ambapo hadi sasa tumeshafanya matibabu ya upasuaji macho 412 bado tuna siku mbili kwa ajili ya kuendelea kutoa huduma hii," amesema Bw. Lemilia.

Aidha, amesema huduma hiyo inawafikia watu wote wanaoishi katika mkoa wa Songwe huku kukiwa na usafiri wa kuwachukua walengwa na kuwaleta katika Hospitali hiyo baada ya kutambulika na wahudumu wa afya ngazi ya jamii.

Kwa upande wake Meneja wa Kambi hiyo ambaye ni Daktari Bingwa wa macho na Dkt. Stephen Nyamsaya amesema mtoto wa jicho ni ugonjwa ambao unasababisha kuleta mabadiliko ndani ya kioo cha jicho na kusababisha upungufu wa kuona.

"Kila mtu anazaliwa na kioo cha kawaida ndani ya jicho ambacho ni cheupe kinachoruhusu mwanga kupita inakuwa kama ni lenzi ya jicho, kadiri umri unapoongezeka husababisha tatizo hilo lakini ugonjwa huu unatibika," amesema Dkt. Nyamsaya.

Naye, Daktari Bingwa wa Macho kutoka Hospitali ya Kanda Mbeya Dkt. Ally Magero amesema zaidi ya asilimia 70-80 wameona vizuri kwa kile kiwango kinachohitajika kuona na wengine wataendelea kuona vizuri kadiri wanavyoendelea kutumia dawa wanazopewa baada ya upasuaji.

Pia ametoa wito kwa Watanzania (vijana kwa wazee) kufika kwenye vituo vinavyotoa huduma za matibabu ya macho kwakuwa ugonjwa wa mtoto wa jicho unatibika huku akiwaasa wazee kuwa sio kawaida ukifika uzeeni kuwa na changamoto ya kuona.