Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WANAFUNZI ZAIDI YA 1,200 WANUFAIKA NA ELIMU YA AFYA YA MACHO

Posted on: October 9th, 2025

Na WAF – Dodoma


Maadhimisho ya Siku ya Afya ya Macho Duniani yamefanyika kitaifa kwa kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule za msingi, hatua inayolenga kuongeza uelewa kuhusu namna ya kujikinga na matatizo ya macho.


Akizungumza katika maadhimisho hayo leo Oktoba 09, 2025, Afisa kutoka Mpango wa Taifa wa Huduma za Macho, Idara ya Tiba Wizara ya Afya, Dkt. Eunice Headcraph, amesema uamuzi wa kutoa elimu kwa watoto wa shule za msingi unatokana na ukweli kwamba kundi hilo ndilo lenye changamoto kubwa zaidi za matatizo ya macho.


“Tumetoa elimu hii kwa wanafunzi 1,213 kuhusu namna bora ya kujikinga na kuchukua tahadhari mapema endapo dalili za matatizo ya macho zitajitokeza,” amesema Dkt. Eunice.


Amesema maadhimisho haya hufanyika kila Alhamisi ya pili ya mwezi Oktoba kila mwaka, yakilenga kuhamasisha jamii kuchukua hatua za kujilinda dhidi ya magonjwa ya macho na kuhakikisha huduma za afya ya macho zinapatikana kwa wote.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Asasi Zisizo za Kiserikali zinazoshughulikia Huduma za Macho nchini, Bw. Eden Mashayo, amesema wao kama wadau wameungana na Serikali katika kutoa elimu hiyo ili jamii iwe na uelewa mpana kuhusu matumizi sahihi na utunzaji wa macho.


“Ushirikiano wetu na Serikali una lengo la kuhakikisha wananchi wote wanapata elimu ya afya ya macho na wanachukua hatua sahihi za kujikinga,” amesema Bw. Mashayo.



Jicho ni moja ya viungo nyeti ndani ya mwili, ambapo kupoteza uwezo wa kuona kunaweza kumfanya mtu kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kila siku ya kujitafutia riziki.