Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WADAU WATAKIWA KUUNGA MKONO BUNIFU ZINAZOSHINDA

Posted on: July 3rd, 2025

Na WAF - DAR ES SALAAM.


Serikali imetoa rai kwa wadau na jamii kuendelea kuunga mkono ukuzaji wa bunifu zilizoshinda kwa kuweka mifumo wezeshi kwa wabunifu hususani katika eneo la uongezaji virutubishi kwenye chakula Ili kuchochea uelewa na uhitaji wa bidhaa zinazoongezwa virutubishi ziwe zinatambulika, zinapatikana kwa kila familia ya Kitanzania.


Rai hiyo imetolewa na  Mkurugenzi Idara ya Mafunzo Wizara ya Afya Dkt. Saitore Laizer wakati akimwakilisha Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama Julai 3, 2025,  Jijini Dar es Salaam katika hafla ya utoaji wa zawadi kwa washindi wa fainali ya shindano la ubunifu wa kuimarisha lishe (FORTIFY FORWARD INNOVATIVE CHALLENGE - EAST AFRICA FINALE - 2025).


Amesema Kupitia juhudi za pamoja zitafungua njia madhubuti na endelevu za kushughulikia upungufu wa virutubishi mwilini (madini na vitamini) kwa kiwango kikubwa.



“Tuendelee kuunga mkono ukuzaji wa bunifu zilizoshinda kupitia Sera, manunuzi na uwekezaji, tuweke mifumo wezeshi ya kifedha kwa ajili ya wajasiriamali wadogo na wa kati na wabunifu katika wigo wa uongezaji virutubishi kwenye chakula ili kuchochea uelewa na uhitaji katika jamii na bidhaa zilizoongezwa virutubishi ziwe zinatambulika, zinapatikana kwa bei nafuu kwa kila familia ya Kitanzania,” amesema Dkt. Saitore.



Dkt. Saitore amesema Utapiamlo bado unaendelea kuathiri  watu  kwa nyanja mbalimbali na urutubishaji wa chakula viwandani na kibiologia siyo tu ni suluhisho la haraka la kiufundi bali ni nyenzo za kimkakati za kuwezesha lishe bora, uchumi imara, na jamii zenye uwezo wa kustahimili changamoto.


Amesema Serikali iko tayari kuwaunga mkono wabunifu wote kupitia miongozo na kanuni bora, mifumo ya kifedha, na mazingira bora zaidi ya ukuzaji wa bunifu na kuwa mwanzo wa kupanua wigo na msaada endelevu. 


“Ni muhimu tuhakikishe kwamba bunifu zilizoshinda hazibaki tu kama majaribio bali zinakuwa nguzo ya kuimarisha biashara zilizopo, kuleta ajira zaidi, kuongeza thamani kwenye kilimo chetu, na kuboresha lishe ya mamilioni ya Watanzania,” amesema Dkt. Saitore 



Nchini Tanzania, asilimia 30 ya watoto chini ya umri wa miaka mitano wamedumaa, na kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2022 (DHIS 2022) upungufu wa damu una athiri zaidi ya asilimia 42 ya wanawake walio kwenye umri wa kuzaa, asilimia 56 ya wajawazito na asilimia 59 ya Watoto chini ya miaka mitano. Kwenye ukanda wetu wa Afrika, 


Ripoti ya afya duniani inaonesha kuwa kiwango cha udumavu  miongoni mwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ni  asilimia 30.7. Kiwango hiki ni juu zaidi ya wastani wa dunia ambao ni asilimia 22.2. Takwimu hizi zinawakilisha na kutukumbusha juu ya athari za lishe duni katika elimu kwa Watoto, afya na uchumi wa nchi zetu kwa ujumla.


Tuzo za shindano la ubunifu wa kuimarisha lishe (FORTIFY FORWARD INNOVATIVE CHALLENGE - EAST AFRICA FINALE - 2025) zimetolewa Mkurugenzi Idara ya Mafunzo Wizara ya Afya Dkt. Saitore Laizer kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama Julai 3, 2025,  Jijini Dar es Salaam, 


Washindi 11 wamepatikana kati ya washiriki zaidi ya  1000 kutoka mataifa nane ya Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Msumbiji, Nigeria, Ethiopia na Benin amabapo kati yao Tanzania imetoa washindi wanne, Kenya wanne na Rwanda watatu.