WADAU, SERIKALI TUSHIRIKIANE KUBORESHA MAZINGIRA YA KUTOLEA HUDUMA ZA AFYA
Posted on: September 10th, 2024NA WAF - DAR ES SALAAM
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. John Jingu ametoa wito kwa Makampuni,Taasisi, Mashirika na jamii kwa ujumla kushirikiana na Serikali kuboresha maeneo ya kutolea huduma za afya.
Dkt. Jingu amesema hayo Septemba 10, 2024 wakati akipokea Shuka zen6e Thamani ya shilingi Milioni 25 kwa ajili ya hospitali sita za rufaa za Mikoa ya Kiafya ambazo zimetolewa na Chama cha Ushirika cha Tanesco (Tanesco Saccos) jijini Dar es salaam kwa Hospitali ya Mwananyamala.
“Kama wanajamii iwe ni kampuni iwe ni shirika lisilo la kiserikali, tunalo jukumu kama jamii kuhakikisha tunashiriki kuviwezesha vituo vyetu kufanya kazi, amesema Dkt. Jingu na kuongeza
"Serikali imefanya kazi na inaendelea kufanya kazi kubwa lakini na sisi mmoja mmoja tuna jukumu, Tukifanya hivyo ni faida kwa wengine na kwetu sote kwakuwa sisi sote ni wateja watarajiwa wa hospitali, kwahiyo tunajukumu sisi sote kuhakikisha hospitali zetu zinakuwa na mazingira mazuri ya kutolea huduma” amesisitiza Dkt. Jingu.
Dkt. Jingu ameongeza kuwa Msaada wa Shuka kutoka Tanesco Saccos ni kiashirio cha kuunga Mkono suala la kuimarisha ubora wa huduma za Afya nchini ambalo ni miongoni mwa ajenda kubwa za Rais Dkt. Samia Sulluhu Hassan.
Aidha Dkt. Jingu ameipongeza Tanesco Saccos kwa kuona haja na umuhimu ka kuisaidia Serikali kuboresha mazinhirabya kutole huduma kwa kutoa mashuka hayo ambapo kwa hi ni awamu ya pili.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tanesco Saccos Edna Mfupa amesema TANESCO Saccos itaendelea na jitihada za kusaidia sekta ya afya nchini na kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Kuhusu mgawanyo shuka hizo Bi Edna amesema Hospitali ya Rufaa Mwananyamala itapata Shuka 200, Hospitali ya Rufaa Temeke Shuka 200, Hospitali ya Rufaa Ilala Shuka 200, Hospitali ya Rufaa Njombe shuka 150, Hospitali ya Rufaa Simiyu Shuka 150, Hospitali ya Rufaa Katavi shuka 150.