Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TANZANIA, COMORO KUENDELEA KUSHIRIKIANA KWENYE SEKTA YA AFYA

Posted on: October 12th, 2025

Na WAF – Comoro


Serikali ya Tanzania na Comoro zimeahidi kuendelea kushirikiana na ili kuimarisha sekta ya afya, ikiwepo kutoa mafunzo kwa wataalam wa afya na kubadilishana uzoefu wa kitaalam.


Ahadi hiyo imetolewa na Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Mhe. Saidi Yakubu, Oktoba 11, 2025 wakati wa hafla ya kufunga Kambi ya matibabu iliyofanyika katika Hospitali ya Bambao, ambapo jumla ya wananchi 3,653 walihudumiwa na kati yao wagonjwa 20 walifanyiwa upasuaji uliookoa maisha yao.


Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Gavana wa Kisiwa cha Anjouan, Dkt. Zaidou Youssouf, akiwa na Mshauri wa Rais wa Comoro (Siasa), Mhe. Humed Msaidie, ameahidi kufanya ziara ya kutembelea Tanzania mwezi Januari 2026 kwa ajili ya kuimarisha makubaliano ya ushirikiano kati ya nchi hizi mbili, hususan katika uratibu wa kesi za rufaa za wananchi wa Anjouan.


Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Asha Mahita, amesema kuwa maeneo ya ushirikiano kati ya Tanzania na Comoro yanajumuisha mafunzo kwa wataalamu, usambazaji wa dawa na vifaa tiba, sambamba na uimarishaji wa huduma za kibingwa na Ubingwa bobezi.


Kambi hiyo ya matibabu ilihusisha madaktari 52 kutoka taasisi mbalimbali nchini Tanzania zikiwemo Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), pamoja na Bohari Kuu ya Dawa (MSD).


Ushirikiano huo unaendelea kudhihirisha dhamira ya Tanzania kuunga mkono juhudi za kuimarisha huduma za afya kwa ukanda husika kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, nafuu na zenye ubora wa kimataifa.