SERIKALI YATAMBUA MCHANGO WA WATOA HUDUMA ZA AFYA KUPIGANIA AFYA ZA WANANCHI
Posted on: July 30th, 2025
NA WAF – DAR ES SALAAM
Serikali imeendelea kutambua na kuthamini mchango mkubwa wa watoa huduma na wahudumu wa Sekta ya afya kwa kuendelea kuwa kiungo muhimu katika kulinda na kupigania afya za Watanzania.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, Julai 30, 2025, wakati wa ziara yake katika Taasisi ya Mifupa, Mishipa ya fahamu na Upasuaji wa Ubongo (MOI), jijini Dar es Salaam.
Akiwa katika ziara hiyo Dkt. Shekalaghe ametuma salamu hizo kwa watumishi na watoa huduma na wataalam wa Sekta ya afya nchi nzima kutokana na namna wanavyojitoa kwa moyo, licha ya changamoto wanazokutana nazo katika kutekeleza majukumu yao.
“Utendaji kazi wenu ni mzuri sana na tunajivunia sana huko wizarani. Hongereni mno mnafanya kazi nzuri sana. Sisi kama Wizara tunathamini sana mchango wenu. Wananchi pia wanasifia ubora wa huduma mnazotoa,” amesema Dkt. Shekalaghe.
Ameongeza kuwa Serikali inatambua mchango wa kila mtoa huduma katika sekta ya afya, kuanzia ngazi ya msingi hadi taifa, na itaendelea kutoa motisha kadri itakavyoweza ili kuongeza ari na ufanisi katika utoaji wa huduma.
Aidha, amewahimiza watumishi wa afya kuendelea kuwahudumia wananchi kwa haki, usawa, huruma na upendo, jambo ambalo litazidi kuimarisha uhusiano bora kati ya wahudumu na wananchi.
“Tuyafanyie kazi yale mapungufu madogo kabla hayajakua na kusababisha malalamiko kwa wananchi, Tujikite katika kuzizuia changamoto hizo kwa kusikiliza na kuzitatua kwa haraka na niwaombe muendelee kuwahudumia wananchi kwa haki, ili kuipa thamani kazi kubwa anayofanya Mhe. Rais kwa ajili ya sekta ya afya,” ameongeza Dkt. Shekalaghe.