Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI YAPANUA HUDUMA ZA CHANJO, TIBA NA ELIMU YA HOMA YA INI

Posted on: January 29th, 2026

Na WAF, Dodoma


Serikali imeendelea kuboresha huduma za afya kwa kuimarisha kinga dhidi ya ugonjwa wa Homa ya Ini kupitia utoaji wa chanjo bure kwa watoto pamoja na chanjo kwa watu wazima, ikiwa ni hatua ya kuzuia maambukizi mapya ya ugonjwa huo.


Hayo yameelezwa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, wakati akijibu swali la nyongeza la Mhe. Naomy Dungan Mwaipopo (Viti Maalum) leo Januari 29, 2026 Bungeni jijini Dodoma, aliyeuliza mkakati wa serikali wa kuhakikisha ugonjwa wa homa ya ini unatokomezwa.


Aidha, Dkt. Samizi amesema Serikali imeanzisha huduma za tiba ya magonjwa ya ini, ambapo kuanzia Desemba 2025 hospitali zote za mikoa, kanda na taifa zimeanza kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya ugonjwa wa Homa ya Ini ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hizo karibu na maeneo yao.


Katika hatua nyingine, amesema Serikali imeeleza kuwa itaongeza juhudi za usimamizi shirikishi katika mikoa inayoongoza kitaifa kwa viwango vya maambukizi ya ugonjwa wa Homa ya Ini, kwa lengo la kudhibiti na hatimaye kutokomeza ugonjwa huo katika mikoa iliyoathirika zaidi.


Pia, Dkt. Samizi ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi kupima ugonjwa wa Homa ya Ini mapema ili kuchukua tahadhari stahiki, kujikinga dhidi ya maambukizi, pamoja na kupata matibabu kwa wakati.


Aidha, huduma hizo jumuishi zimeendelea kuboreshwa kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI, Magonjwa ya Zinaa na Homa ya Ini (NASHCoP), ambapo wahudumu wa afya wamepatiwa miongozo na maelekezo ya kitaalamu ili kuwawezesha kutoa huduma bora na salama kwa wananchi.