SERIKALI YAJIZATITI KUKABILIANA NA MARBURG
Posted on: January 26th, 2025
Serikali imeendelea na jitihada za kudhibiti ugonjwa wa Marburg nchini tangu ulipotangazwa kuwepo wilayani Biharamulo mkoani Kagera, kwa mara ya kwanza Januari 19, 2025 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mkurugenzi wa Kinga wa Wizara ya Afya Dkt. Ntuli Kapologwe amebainisha hayo leo Januari 24, 2025 wilayani Biharamulo wakati akitoa taarifa ya kamati ya kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa Marburg katika Hamashauri ya wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera kwa Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe aliyefika wilayani hapo kujionea hali halisi.
Dkt. Kapologwe amesema tangu kutangazwa kwa ugonjwa huo Januari 19, 2025 Wizara ya Afya imepiga kambi wilayani humo na kutoa huduma kwa wahisiwa wa ugonjwa huo sambamba na kutoa elimu kwa wananchi jinsi ya kujikinga ba ugonjwa pamoja na kutambua dalili za ugonjwa huo ambao mpaka sasa idadi ya waliofariki ni wawili, wagonjwa wahisiwa imefikia 15 huku wale waliokuwa jirani na walioathirika wa Marburg kufikia 281.
“Serikali imeimarisha udhibiti wa ugonjwa huu, kwa kuwaleta madaktari bingwa, vifaa ya upimaji, madawa pamoja na kuwatumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii ambao wamekuwa wakipita nyumba kwa nyumba kuwabaini washukiwa wa ugonjwa huo,” amesema Dkt. Kapologwe.
Dkt. Kapologwe amesema wametembelea kaya zote 10,893 ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo ambapo Kata mbili kati ya 17 za Halmashauri hiyo ndizo zimeathirika na ugonjwa huo.
Dkt. Kapologwe amesema maeneo 13 yametengwa kwa ajili ya wananchi waliokuwa karibu na waathirika ambao kati ya hao 64 ni watumishi wa afya.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe ameshukuru kwa jitihada zinazofanywa na wataalam hao kwa kushirikiana uongozi wa wilaya na kusisitiza kuwa utoaji wa elimu kwa wananchi ni muhimu katika kipindi hiki ili kujua wafanye nini ili kuwa salama.
Aidha Dkt. Magembe amewataka wananchi kutoa taarifa mapema katika vituo vya tiba pindi wanapoona kitu chochote ambacho si cha kawaida pamoja na kuwasihi wahudumu wa afya kuzingatia uvaaji wa mavazi ili kujikinga na maradhi.