Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI, WHO, KUWA NA MPANGO KAZI WA PAMOJA KUIMARISHA HUDUMA ZA AFYA NCHINI

Posted on: November 20th, 2025

Na WAF, Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) wameazimia kuja na mpango kazi wa pamoja wa miaka miwili wa kuimarisha huduma za afya nchini.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe leo Novemba 20, 2025 Jijini Dodoma wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha kwa pamoja wataalam wa Sekta ya Afya kutoka Wizarani na WHO.

“Tunahitaji kuwa na mpango kazi ambao unaendana moja kwa moja na vipaumbele vya Taifa, ikiwemo mpango mkakati wa miaka mitano na bajeti ya mwaka wa fedha, ili kupata matokeo yaliyoratibiwa kitaifa,” amesema Dkt. Shekalaghe.

Pia Dkt. Shekalaghe amesema Tanzania imekuwa na historia ndefu ya mafanikio katika sekta ya afya, hivyo katika mipango mipya ya uboreshaji huduma za afya nchini ni vyema ifuate misingi ya uongozi na utendaji iliyoijengea nchi heshima Barani Afrika.

“Historia yetu ni ushahidi kuwa tukijipanga vizuri, tunafanya vizuri, sasa tunahitaji kufanya zaidi na kwa ubora zaidi,” amesema Dkt. Shekalaghe.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani nchini Tanzania Dkt. Alex Gasasira amesema kuwa mpango huo wa pamoja ni lazima uwe unaongozwa na nchi yenyewe badala ya kutungwa kutoka nje kwani kama nchi tayari ina vipaumbele vyake katika Sekta ya Afya.