Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI KUENDELEA KUTOA KIPAUMBELE KWA WATOTO WA KIKE ILI KUJENGA JAMII YENYE USAWA

Posted on: October 11th, 2022

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kutoa kipaumbele katika kuhakikisha wanawake na watoto wa kike wanapata huduma wezeshi zikiwemo za afya na elimu ili kuwezesha kujenga jamii yenye usawa.
Ameyasema hayo (Jumanne, Oktoba 10, 2022) alipomuwakilisha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa Viongozi wa Ngazi za Juu ya Kuwezesha Viongozi Wakuu juu ya Kuwezesha Vipaumbele vya Wanawake na Wasichana katika Mapambano Dhidi ya Virusi Vya Ukimwi uliofanyika Serena Hoteli jijini Dar Es Salaam.
 
“Wasichana wakipata elimu bora wataweza kuepukana na maambukizi ya virsri vya ukimwi, kuanzia katika ngazi ya familia na jamii kwa ujumla, hivyo ni wajibu wetu kuwekeza kwa watoto wa kike ili kuwa na jamii yenye mafanikio na usawa katika maendeleo.” Amesema Mhe. Kassim Majaliwa.
 
Amesema kuwa Serikali imechukua hatua mbalimbali katika kuhakikisha wanaweka kipaumbele katika kuwahudumia wanawake wanaoishi na VVU ikiwemo kuviwezesha vikundi vyao, kutoa elimu pamoja na kuwajumuisha katika ngazi za maamuzi kwenye sehemu za kutolea huduma za afya.

Waziri Mkuu amesema katika kufanikisha mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi ni vyema watoto wa kike wakapewa nafasi katika utungaji wa Sera na miongozo ya kupambana na ugonjwa huo itaongeza ufanisi katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo kwani kundi hilo limekuwa sehemu ya waathirika wakubwa.
 
Kwa upande wake Waziri wa Afya Mhe. @ummymwalimu amempongeza Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa kwa kuwa kuwa kinara katika kuongoza mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi.
 
Waziri Ummy amelishukuru Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Wanawake (UN WOMEN) Serikali ya Marekani kupitia PEPFAR pamoja na Global Fund pamoja na wadau wengine kwa kuwezesha utekelezaji wa afua za mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi pamoja na Kifua Kikuu.
 
Waziri Ummy amesema kuwa kupitia kikao hicho nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara zitaweka mikakati ya pamoja ili kusonga mbele katika kumkomboa mtoto wa kike na wanawake kwa ujumla pamoja kuweka mikakati ya kuwalinda dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.

Mwisho.