Wizara Ya Afya

HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA NJOMBE KUANZA KUTOA HUDUMA ZA USAFISHAJI WA DAMU KWA WAGONJWA WA FIGO

Posted on: July 7th, 2026

Na Shaban Juma, WAF – Njombe

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe imeanza kutoa huduma za usafishaji wa damu kwa wagonjwa wa figo (Dialysis), ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Waziri wa Afya, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, ya kuhakikisha hospitali zote za rufaa za mikoa nchini zinaanzisha huduma hiyo ili kupunguza adha ya wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu.

Hayo yamebainishwa na leo Julai 07, 2026 na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, kwa niaba ya Waziri wa Afya, wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Njombe ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya sekta ya afya pamoja na utoaji wa huduma kwa wananchi.

Dkt. Samizi amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi katika hospitali za umma kwa kusogeza huduma muhimu karibu na wananchi, hatua inayopunguza gharama na muda wa kupata matibabu.

"Maelekezo ya Waziri wa Afya ni kuhakikisha kila Hospitali ya Rufaa ya Mkoa inaanzisha huduma za usafishaji wa damu kwa wagonjwa wa figo ili wananchi wasilazimike kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo. Njombe muanze, na hospitali nyingine ambazo bado hazijaanza zinapaswa kuharakisha maandalizi na kuanza kutoa huduma hizi muhimu," amesema Dkt. Samizi.

Aidha, amezitaka hospitali zote za rufaa za mikoa ambazo bado hazijaanza kutoa huduma za dialysis kuhakikisha zinakamilisha maandalizi yote muhimu ikiwemo miundombinu, vifaa tiba na rasilimali watu ili wananchi waweze kunufaika na huduma hizo katika maeneo yao.

Kwa upande wake Mganga mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe ameeleza kuwa mpaka sasa mashine 12 zimefungwa huku akibainisha kuwa kuanza kwa huduma hiyo kutapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto zilizokuwa zikiwakabili wagonjwa wa figo waliokuwa wakilazimika kusafiri kwenda mikoa mingine kupata matibabu, huku ukiahidi kuendelea kuboresha ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.