DKT. MAGEMBE: MSHIKAMANO WA WATUMISHI NI MSINGI WA HUDUMA BORA ZA AFYA
Posted on: July 6th, 2026Na Zakayo Mosha – WAF, Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, amewataka watumishi wa sekta ya afya nchini kudumisha mshikamano, upendo na ushirikiano mahali pa kazi ili kuongeza ufanisi wa utendaji na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Dkt. Magembe ametoa wito huo leo Julai 6, 2026, alipowasili kwa mara ya kwanza katika Ofisi za Wizara ya Afya Mtumba jijini, Dodoma, mara baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo Juni 26, 2026 na kuapishwa Julai Mosi, 2026 kushika wadhifa huo.
Dkt. Magembe amesema mafanikio ya wizara yanategemea ushirikiano wa watumishi wa ngazi zote, kuanzia halmashauri, mikoa hadi makao makuu ya wizara, akisisitiza kuwa kila mmoja anapaswa kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kwa kushirikiana na wenzake.
“Naomba kila mmoja wetu atimize wajibu wake kwa kuzingatia nidhamu, uadilifu, uzalendo, utu na uwajibikaji mahali pa kazi. Pia tufanye kazi kwa usawa bila kusukumwa au kusimamiwa kwa karibu na viongozi wetu,” amesema Dkt. Magembe.
Dkt. Magembe ametumia nafasi hiyo kumshukuru, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa imani aliyompa kwa kumteua kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, akiahidi kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu na kuhakikisha wizara inaendelea kusimamia utoaji wa huduma bora za afya.
Katika hatua nyingine, amewataka Viongozi wa idara na vitengo kuhakikisha wanasimamia haki, maslahi na ustawi wa watumishi kwa usawa ili kuongeza tija na ufanisi kwa kupunguza malalamiko na kuimarisha utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.