Wizara Ya Afya

DKT. SAMIZI AHIMIZA UWAJIBIKAJI, ASISITIZA KUKAMILIKA KWA JENGO LA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA RUVUMA

Posted on: July 6th, 2026

Na Shaban Juma – Songea, Ruvuma

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesema Serikali inahitaji takribani shilingi bilioni 4.5 kukamilisha ujenzi wa jengo jipya la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma ili kuongeza uwezo wa hospitali hiyo kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa hospitali hiyo mkoani Ruvuma kwa niaba ya waziri wa afya Mhe. Mohamed Mchengerwa, Dkt. Samizi amesema kukamilika kwa jengo hilo kutasaidia hospitali kupanua huduma za kibingwa kutoka huduma nane zinazotolewa kwa sasa kuelekea kufikia huduma 16 zinazotakiwa kwa hospitali za rufaa za mikoa.

Amesema Serikali ina kila sababu ya kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati ili wananchi wa Ruvuma na mikoa jirani waendelee kupata huduma za kibingwa karibu na maeneo yao na kupunguza rufaa zisizo za lazima kwenda hospitali za ngazi ya juu.

Katika hatua nyingine, Dkt. Samizi amezungumza na watumishi wa hospitali hiyo na kuwataka kuendelea kuwajibika ipasavyo katika utekelezaji wa majukumu yao, akisisitiza kuwa msingi wa huduma bora za afya ni uwajibikaji, weledi na maadili ya kazi.

Amesema kipimo halisi cha ubora wa huduma za afya hakitokani na takwimu pekee, bali kinapimwa na kiwango cha kuridhika kwa wananchi wanaopokea huduma hizo. Hivyo, amewataka watumishi kuwahudumia wananchi kwa heshima, utu na weledi ili kuongeza imani ya wananchi kwa huduma zinazotolewa na Serikali.

Dkt. Samizi amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuboresha miundombinu ya afya, vifaa tiba na mazingira ya kazi ya watumishi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, salama na zenye ubora unaokidhi mahitaji yao.