Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

DKT.SHEKALAGHE AIAGIZA OCEAN ROAD KUKAMILISHA UFUNGAJI WA PET SCAN

Posted on: November 25th, 2025

Na. WAF, Dar es Salaam


Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, ameuagiza Uongozi wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na mkandarasi anayesimika kifaa tiba cha PET Scan kuhakikisha wanakamilisha usimikaji wa kifaa hicho ndani ya muda waliokubaliana.


Dkt. Shekalaghe ametoa maagizo hayo Novemba 25, 2025, wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa utoaji wa huduma katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, jijini Dar es Salaam.


“Tumekubaliana kwamba hadi siku ya Ijumaa, mkandarasi anatakiwa kumpatia Mkurugenzi wa Ocean Road uhakiki wa benki (Bank Guarantee) ili Mkurugenzi aweze kumlipa asilimia 75 ya malipo yake. Hii itamwezesha mkandarasi kufanya maandalizi ya kuhakikisha PET Scan inaanza kufanya kazi. Wataalam wamenishauri kuwa baada ya hapo tutahitaji siku 30 kwa ajili ya maandalizi ya mashine hiyo kuzalisha mionzi tiba kwa ajili ya kugundua kansa,” amesema Dkt. Shekalaghe.


Aidha, amewahakikishia wananchi wanaofika hospitalini hapo kupata huduma, kuwa Serikali imenunua galimu mbadala ambayo itasaidia mashine ya PET Scan kufanya kazi wakati maandalizi ya mwisho ya ufungaji wake yakiendelea.


Ameongeza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa Shilingi Bilioni 60 kuboresha huduma za afya katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road kwa kununua vifaa tiba vya kisasa na kujenga jengo la PET Scan, hatua ambayo inalenga kuokoa maisha ya Watanzania wengi.


“Fedha hizo zimetumika kujenga jengo la PET Scan, kununua PET Scan, mashine mbili za Cobalt, mashine ya Linac, MRI na CT Scan ndani ya miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia katika awamu ya kwanza. Yote haya ni kutokana na mapenzi yake kwa wananchi wa Tanzania,” amesema Dkt. Shekalaghe.


Amebainisha kuwa ugonjwa wa kansa ni miongoni mwa magonjwa ambayo Mheshimiwa Rais ameelekeza yapewe kipaumbele kupitia Bima ya Afya kwa Wote, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bila vikwazo vya kifedha. 


Aidha, amesema wananchi wote wenye magonjwa sugu watatibiwa bila kujali hali zao za kiuchumi mradi wanachangia kwenye bima ya afya.