Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

BARAZA LA FAMASI SIMAMIENI TAALUMA IPASAVYO-WAZIRI MHAGAMA

Posted on: December 19th, 2024

Na WAF - Dodoma

Balaza jipya la Famasi nchini limetakiwa kusimamia kwa weledi taaluma ili kuleta tija na ufanisi kwenye utendaji.

Rai hiyo imetolewa Desemba 17, 2024 na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama wakati wa hafla ya uzinduzi wa Baraza jipya la Famasia lililoteuliwa na kuliaga lililomaliza muda wake.

"Jukumu kubwa la Baraza ni kuleta msukumo katika utoaji wa huduma bora za kifamasia ili kuweza kulinda afya za Watanzania," amesema Waziri Mhagama.

Mhe. Mhagama amesema Baraza lililopita lilifanya kazi kubwa ikiwa ni pamoja na kusajili wafamasia 3,725, fundi dawa sanifu 8,635, fundi dawa wasaidizi 1028, famasi 3040 pamoja na maduka ya dawa muhimu 22,213.

"Miaka Ishirini Iliyopita Baraza hili lilikuwa na watumishi wawili (2) na hadi kufikia mwaka 2024 kumekuwa na ongezeko la idadi ya watumishi ambao wamefikia 56," amefafanua Mhe. Mhagama.

Waziri Mhagama ametumia wasaa huo kupongeza juhudi za Baraza kwa kukamilisha ujenzi kwa kutumia vyanzo vya mapato ya ndani bila kutegemea msaada.

Akizungumza katika hafla hiyo Mfamasia Jafari Liana ambaye ni Mwenyekiti mpya wa Baraza hilo amesema, wamepokea maelekezo ya Serikali na kuahidi kuendeleza na kutekeleza yote waliyoshauriwa.

Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Ahmad Makuwani amesema, mabaraza yanatakiwa kufanya kazi kwa umoja ikiwepo, Baraza la Famasia, Uuguzi na Ukunga pamoja na lile la Madaktari.

Baraza jipya la Famasia linaundwa na Jafari Liana (Mwenyekiti), wajumbe wakiwa ni Bw. Daudi Msasi, Dkt. Ritah Mtagonda, Bw. Fadhili Hezekiah, Bw.Thabiti Milandun, Bw. Masha Mkata na Bi.Rehema Katuga.