WATAALAM WA AFYA TUMIENI TAKWIMU KUCHECHEMUA UBORA WA HUDUMA
Posted on: July 18th, 2024
Na WAF – KIGOMA
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu amewataka wataalamu wa Afya nchini kutumia takwimu na tafiti mbalimbali kama kiongozo cha kusaidia kutambua na kutatua chagamoto zinazoikabili sekta ya Afya katika maeneo yao ya kiutendaji ili kufikia lengo la Serikali la kuimarisha zaidi ubora wa huduma za Afya nchini.
Prof. Nagu amesema hayo Julai 18, 2024 wakati akiendelea na ziara yake Mkoani Kigoma katika Wilaya ya Buhigwe ambapo ametembelea Hospitali ya Wilaya hiyo kujionea hali ya utoaji wa huduma za Afya na ujenzi wa miradi ya maendeleo.
Prof. Nagu amesema bila kutumia takwimu haitawezekana kujua changamoto jambo litakalopelekea ugumu pia katika kutatua changamoto na kuboresha hali ya utaji wa huduma za afya nchini.
Amesema kupitia takwimu ameona jinsi wilaya hiyo ilivyojifanyia tathimini na kujifanyia maboresho katika kudhibiti vifo vya wakina mama wajawazito na watoto wachanga vitokanavyo na uzazi ambapo awali 2021 vilikuwa vifo 7 vya wakina mama wakati kwa mwaka huu mpaka sasa ni Kimoja pekee na kwa upande wa watoto wachanga vilikuwa vifo 48 na sasa ni vifo 12 pekee
Prof. Nagu amepongeza pia Wilaya ya Buhigwe kwa kuimarisha mapambano dhidi ya magonjwa ya mlipuko maeneo ya mpakani licha ya kuwa na eneo kubwa la mpaka.
“Pamoja na kuwa mna eneo la mpaka kubwa lakini niwapongeze mpaka sasa hakuna magojwa ya mlipoko hakuna Surua, Kipindupindu na mengineyo pamoja ya kwamba apa tunajua ni mpakani na mpaka mkubwa wa Burundi, kwasababu naangalia changamoto na mnazifanyia kazi na mnatatua, hii ni mfano wa kutumia takwimu kufanya maamuzi “ Amesema Prof. Nagu
Awali akisoma taarifa ya hospitali ya Wilaya ya Buhigwe Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Baraka Kemero amesema Halmashauri hiyo ilipokea Fedha Tsh. million 800 kwa ajili ya kujenga majengo ya wodi ya Wanaume, wodi ya wanawake na wodi ya watoto, jengo la kuhifadhia maiti ambapo ujenzi wa wodi hizo umekamilika kwa asilimia zaidi ya 90 na unatarajia kuwanufaisha zaidi ya wananchi 254,342.
Kwa upande wake Mgaanga Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Dkt. Innocent Mhagama amesema Kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kupanua huduma za afya zilizoboreshwa kwa wakazi wa Wilaya ya Buhigwe na kuvutia watu kutoka nchi jirani Pia utasaidia kupunguza adha kwa wanabuhighwe kwenda hospitali za mbali, kupunguza gharama za matibabu na vifo
MWISHO