WAHUDUMU WA AFYA NGAZI YA JAMII 11,515 KUANZA MAFUNZO SEPTEMBA 30,2024
Posted on: September 19th, 2024
Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais -Tamisemi itatoa mafunzo rasmi ya kuwajengea uwezo watoa huduma za Afya ngazi ya jamii 11,515 kuanzia Septemba 30, 2024 ili kufanikisha azma ya Mpango Jumuishi wa wahudumu hao na kuendeleza afua jumuishi za Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama Septemba 19,2024 ofisi ndogo za Wizara ya Afya NIMR Jijini Dar es Salaam, wakati akitoa taarifa kwa umma juu ya kuanza rasmi kwa mafunzo ya Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii kwa mikoa 11 ya Tanzania Bara.
Waziri Mhagama amesema mpango huo utaanza kwenye Halmashauri 21 ndani ya mikoa 11 katika awamu ya kwanza
“Mikoa ambayo itafikiwa na huduma hii kwa Awamu ya kwanza ni pamoja na Geita, Pwani, Tanga, Songwe, Mbeya, Lindi, Tabora, Kagera, Njombe, Ruvuma, na Kigoma" ameainisha waziri Mhagama na kuongeza kuwa
"mpango huu umelenga na unahitaji kuwa na wahudumu wawili wa jinsia ke na me kila mtaa na kila kitongoji, uchaguzi wa wahudumu hao umeshirikisha wananchi na wana jamii kutoka kitongoji husika au mtaa husika.”Amefafanua Waziri Mhagama
Wakati wa utoaji wa mafunzo amesema yatatolewa kupitia Vyuo vya Afya vya Kada ya Kati kwa kipindi cha miezi sita, ambapo miezi mitatu ya awali mafunzo yatatolewa kwa njia ya nadharia na miezi mitatu iliyobaki mafunzo yatakuwa kwa njia ya vitendo katika maeneo yao ili kuongeza umahiri kwa wahudumu kuweza kutekeleza kwa uhalisia kile walichojifunza.
Waziri Mhagama amesema jumla ya wanajamii 31,275 walijitokeza kuomba nafasi huku wanajamii elfu 21,574 waliokidhi vigezo kwenye hatua ya awali walichaguliwa.
“Kwa awamu ya kwanza zoezi la kuwachagua wahudumu wa afya Ngazi ya Jamii lilifanyika kati ya tarehe 08/06/2024 hadi 25/07/2024 kwenye Halmashauri 21 kwa mikoa kumi na kuleta idadi ya waliokidhi vigezo elfu 21,574 na huku Mkoa wa Ruvuma wahudumu elfu 1,227 wanachaguliwa ili kuwa na jumla ya Wahudumu elfu 11,515 ”Amesema Waziri Mhagama
Waziri Mhagama hakusita kuonya wale wote watakaotaka kujinufaisha na zoezi hilo na kuonya kuwa Wizara ya Afya itachukua hatua kali kwa yeyote atakaejaribu kutengeneza mavazi ambayo yatakuwa sawa na mavazi ambayo watayatumia waudumu wetu na kujifanya ni wahudumu wa afya”Amesema Waziri Mhagama
Mpango huu ulihusisha jumla ya mitaa elfu 1044, vijiji 754, na vitongoji elfu 3,853 baada ya uchaguzi kupitia mikutano ya jamii jumla ya wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii elfu 9,492 walichaguliwa