VITUO BINAFSI VINAVYOOMBA USAJILI VYATAKIWA KUKIDHI VIGEZO VYA UTOAJI HUDUMA BORA ZA AFYA
Posted on: March 6th, 2025
Na WAF - Dar es Salaam
Bodi ya Ushauri wa Hospitali Binafsi imeagizwa kuhakikisha Vituo vinavyoomba usajili vinakidhi vigezo vyote vya utoaji wa huduma bora za Afya kabla ya kupatiwa usajili pamoja na kufuatilia vituo vyote ambavyo vinatoa huduma bila usajili.
Akizungumza wakati uzinduzi wa Bodi Mpya ya 11 ya Hospitali Binafsi leo Machi 5, 2025 Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema, kwa kufanya hivyo watapunguza malalamiko na changamoto kwa wananchi.
Bodi hiyo mpya ya 11 ya ushauri yenye wajumbe sita inaongozwa na Mwenyekiti Dkt. Grace Magembe ambaye ni Mganga Mkuu wa Serikali.
"Bodi hii pia, ina jukumu kubwa la kufanya ukaguzi wa Vituo vya Afya vilivyosajiliwa na kuhakikisha vinatoa huduma bora za afya kwa wananchi kwa kuzingatia ngazi ambayo kituo husika kimesajiliwa, vituo ambavyo vinakiuka miongozo ya utoaji huduma iliyowekwa na Wizara vichukuliwe hatua zinazostahili bila kuogopa," amesema Waziri Mhagama.
Aidha, Waziri Mhagama ameitaka bodi hiyo mpya kufanya kazi kwa karibu na Sekta Binafsi kwa kuwa sekta hiyo ni mshirika wa Serikali na sio mshindani kwa kuwa lengo kubwa ni kuhakikisha mwananchi anapata huduma bora za afya zenye viwango bora na kwa wakati.
"Sisi kama Serikali, tunao wataalam, viongozi, wakaguzi na wasimamizi, wote kwa pamoja tufanye kazi kwa kusimamiana, na yeyote atakayejaribu kuharibu mifumo yetu lazima tushughulike naye, kwani tumeshakubaliana kuwa Sekta Binafsi sio mshindani bali ni mshirika," amesema Waziri Mhagama.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi hiyo Dkt. Grace Magembe amesema kuwa Bodi hiyo ina jukumu la kusajili na kusimamia vituo binafsi vinavyotoa huduma za Afya kote nchini (Tanzania Bara).
"Hadi sasa, Bodi imesajili vituo binafsi vinavyotoa huduma za Afya vipatavyo 3,471 na hii inaonesha wazi mchango wa Sekta Binafsi kwa Serikali katika kuhakikisha huduma bora za Afya zinafika kwa jamii," amesema Dkt. Magembe.