Wizara Ya Afya

UWEKEZAJI KATIKA LISHE BORA NI MUHIMU KUKABILI MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA - PROF. SUNGUYA

Posted on: November 16th, 2026

Na Aisha Swahib, WAF – Dar es Salaam

Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Bruno Sunguya, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha uwekezaji katika lishe bora na tafiti za kisayansi ili kukabiliana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza na changamoto za lishe zinazoendelea kuathiri jamii.

Prof. Sunguya ameyasema hayo leo, tarehe 16 Novemba 2026, wakati wa ufunguzi wa Mkutano Kimataifa wa Mpango wa Lishe Bora Duniani uliofanyika mkoani Dar es Salaam, wenye lengo la kuimarisha matumizi ya tafiti na ushahidi wa kisayansi katika kuboresha lishe na afya ya jamii.

Amesema Tanzania inaendelea kukabiliwa na changamoto kubwa za lishe, hivyo kuna umuhimu wa kuongeza uwekezaji katika hatua za kinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza kwa kuhamasisha ulaji unaozingatia lishe bora na mtindo mzuri wa maisha.

Aidha, Prof. Sunguya ameeleza kuwa jamii nyingi hutegemea vyakula vinavyopatikana katika mazingira yao pamoja na mila na desturi za ulaji, hivyo ni muhimu kuzingatia utamaduni na upatikanaji wa vyakula vya asili katika kuandaa mipango ya kuboresha lishe.

Ameongeza kuwa tafiti zinahitajika ili kubaini namna mifumo na tabia za ulaji zinavyobadilika katika makundi mbalimbali ya umri, hatua itakayosaidia kupata taarifa sahihi za kuandaa mikakati ya lishe inayokidhi mahitaji ya kila kundi katika jamii.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha matokeo ya tafiti za kisayansi yanatafsiriwa na kutumika katika utekelezaji wa afua za afya na lishe, ili maarifa yanayopatikana yaweze kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya wananchi.

Prof. Sunguya ametoa wito wa kuimarisha ushirikiano wa kitaifa na kikanda katika tafiti za lishe, kubadilishana uzoefu na kutumia ushahidi wa kisayansi katika kuandaa sera na mikakati endelevu ya kuboresha afya na ustawi wa jamii.