HUDUMA YA KUTOMTENGANISHA MAMA NA MTOTO NJITI KUPUNGUZA VIFO KWA ASILIMIA 25
Posted on: November 16th, 2026Na Shaban Juma, WAF – Dar es Salaam
Serikali imeimarisha utekelezaji wa huduma ya kutomtenganisha mama na mtoto aliyezaliwa kabla ya wakati (Zero Separation), pamoja na kuanza mapema huduma ya kumuweka mtoto kwenye mgusano wa ngozi kwa ngozi na mama yake (Immediate Kangaroo Mother Care – iKMC), inayoweza kupunguza vifo vya watoto hao kwa asilimia 25.
Hayo yamesemwa Novemba 15, 2026, na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence George Samizi, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto Aliyezaliwa Kabla ya Wakati, akieleza kuwa Tanzania imeridhia mapendekezo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu huduma hizo.
Amesema uamuzi huo umezingatia matokeo ya utafiti uliofanyika Tanzania, Ghana, India, Nigeria na Malawi, ulioonesha kuwa kutomtenganisha mama na mtoto wake kunaweza kupunguza vifo vya watoto waliozaliwa kabla ya wakati kwa asilimia 25 ikilinganishwa na wale wanaotenganishwa na mama zao.
Dkt. Samizi amesema Mwongozo wa Taifa wa Huduma kwa Watoto Wachanga wa mwaka 2018 pamoja na michoro ya ujenzi wa wodi za NCU umezingatia umuhimu wa mama na baba kushiriki katika malezi na huduma za watoto wachanga wanapokuwa hospitalini.
Amesema ushiriki wa wazazi ni muhimu katika kuhakikisha watoto waliozaliwa kabla ya wakati wanapata uangalizi unaostahili, huku huduma ya Kangaroo ikisaidia kuimarisha uhusiano wa mama na mtoto na kuboresha matokeo ya matibabu.
Katika hatua nyingine, Dkt. Samizi amesema NCU ya kisasa iliyojengwa na Taasisi ya Doris Mollel katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba imeonesha matokeo chanya ndani ya miezi tisa tangu kuanza kutoa huduma.
Amesema idadi ya watoto waliolazwa katika wodi hiyo imeongezeka kwa takribani asilimia 200, kutoka 183 hadi 542, huku vifo miongoni mwa watoto waliolazwa vikishuka kwa asilimia 64, kutoka watoto 34 kati ya 100 hadi 12 kati ya 100.
Aidha, rufaa za watoto kwenda hospitali nyingine zimepungua kwa asilimia 70 katika kipindi hicho, jambo linaloonesha umuhimu wa kuwa na miundombinu bora na huduma maalumu karibu na wananchi.