ELIMU YA MABUSHA/NGIRIMAJI IWE ENDELEVU – DKT. SAMIZI
Posted on: November 14th, 2026Na Alex Nkondo, WAF - Mlandizi, Pwani
Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Dkt. Florence Samizi, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu ugonjwa wa Mabusha/Ngirimaji ili kuongeza uelewa wa jamii, kuondoa imani potofu na kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa uchunguzi na matibabu.
Dkt. Samizi ameyasema hayo leo, tarehe 14 Novemba 2026, wakati wa kuhitimisha Kambi Maalumu ya Upasuaji wa Mabusha katika Hospitali ya Wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani, ambapo ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuwezesha upatikanaji wa huduma za upasuaji bila malipo ili kupunguza adha kwa wagonjwa na kuboresha ustawi wao.
Katika kambi hiyo, jumla ya wananchi 533 wamefanyiwa uchunguzi, ambapo 315 wamebainika kuwa na Mabusha, huku wagonjwa 182 wakifanyiwa upasuaji na kuruhusiwa kurejea katika maeneo yao ya makazi. Kambi hiyo imewahudumia wananchi kutoka mikoa ya Pwani, Morogoro na Mbeya.
Aidha, Dkt. Samizi amesisitiza umuhimu wa kuimarisha elimu na hamasa kwa jamii, pamoja na kuangalia namna ya kujumuisha huduma za matibabu ya Mabusha katika utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ili kuongeza upatikanaji wa huduma hizo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, Dkt. Rahma Hingora, amesema Wizara ya Afya itaendelea kutumia vyombo mbalimbali vya habari kutoa elimu kuhusu Mabusha/Ngirimaji ili kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwahamasisha kujikinga na kutafuta matibabu kwa wakati.
Naye, Meneja wa Mpango wa Taifa wa Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele, Dkt. Clara Mwansasu, amesema magonjwa hayo huathiri zaidi wananchi wanaoishi katika mazingira magumu na wenye hali duni ya maisha, hivyo Serikali inaendelea kuimarisha huduma za kinga, uchunguzi na matibabu kwa lengo la kutokomeza magonjwa hayo ifikapo mwaka 2030.