Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

UMOJA WA WAMILIKI VITUO BINAFSI VYA AFYA (APHTA), WAPITISHWA KWENYE SHERIA YA BIMA YA AFYA KWA WOTE

Posted on: December 15th, 2023

NA, WAF, Dar es salaam

Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango na Bajeti wa Wizara ya Afya Bw. Lusajo Ndagile, amewapitisha kwenye Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote Umoja wa Wamiliki wa Vituo Binafsi vya Afya nchini (APHTA) ili kupata maoni yao maeneo ambayo yanaweza kufanyiwa maboresho kabla ya kuanza utekelezaji wake.

Bw. Lusajo ameyasema hayo wakati wa kikao cha kupitia Sheria ya Bima ya Afya kwa wote kilichofanyika kwenye Ofisi ndogo za wizara ya Afya jijini Dar es Salaam.

“Sisi kama Wizara ya Afya na kama Serikali jukumu letu kubwa ni kupokea maoni yenu ili kile tulichokifanya tuweze kukiboresha na mwisho wa siku tuweze kumsaidia Mwananchi katika kupata huduma bora za afya na zenye ufanisi.Amesema Lusajo.

Aidha Bw. Lusajo amesema wizara ya Afya iko kwenye mchakato wa kukutana na wadau mbalimbali wa afya na kuwapitishia kwenye sheria ya Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote ambayo imesainiwa hivi karibu  na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na kupokea maoni ya wadau hao, kwa ajili ya maboresho mbalimbali kabla ya kuanza utekelezaji wake.

Akizungumza kwa niaba ya APHTA Mwenyekiti wa Umoja huo Bw. Mahmoud Mringo, ameipongeza Wizara ya Afya kwa  kutambua umuhimu wao, na kuwapa fursa ya kuweza kutoa maoni yao kabla ya kuanza utekelezaji wake.

 “Fursa hii sisi tumeipigania kwa muda mrefu, na kuzaliwa kwa mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote kwetu ni faraja kubwa, hivyo tunategemea kupitia kikao hiki tunategemea ule usisi na uwao utaondolewa na hatimaye tunaenda kuwahudumia Watanzania kwa haki na usawa”alisema  Mringo.

Pia, Bw. Mringo ameiomba Wizara ya Afya na wote watakaohusika na utekelezaji wa mfuko wa bima ya afya kwa wote, kuhakikisha wanafanyia kazi changamoto ambazo Vituo vyao vya Afya vilikuwa vikikutana nazo wakati wa utekelezaji wa bima ya Afya iliyopo, na kuhakikisha ujio wa bima ya Afya kwa wote utekelezaji wake unakuwa ufanisi mkubwa.