TAKWIMU ZA LISHE ZA KILA MWEZI KUSAIDIA KUMALIZA TATIZO LA UTAPIAMLO.
Posted on: February 12th, 2024
Na WAF - Dodoma
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe amesema uwepo wa takwimu za hali ya Lishe kila Mwezi zitasaidia Serikali na wataalamu wa masuala ya lishe nchini kukabiliana na kuboresha hali ya lishe nchini hasa kwa akina mama na watoto kabla hawajaingia kwenye changamoto kubwa ya utapiamlo.
Dkt Magembe amesema hayo February 12, 2024 wakati alipokutana na Ujumbe kutoka Shirika la UNICEF Tanzania Kwa ajili ya kupokea vitendea kazi vinavyolengwa kusaidia kitengo cha huduma za Lishe ambavyo ni Kompyuta mpakato 10 na projekta moja, katika ofisi za wizara jijini Dodoma.
Dkt. Magembe amesema kipaumbele cha Wizara na Serikali ni kuboresha hali ya lishe kwa kutoa elimu na kuwafikia wananchi wa hali ya chini ambao wengi wao hutumia muda mwingi kutafuta kipato na kushindwa kuzingatia lishe bora.
“Tushirikiane kuhakikisha tunawafikia akina mama wenye watoto wadogo ambao wanaojishughulisha na biashara mbalimbali, wafikiwe na watoa huduma ngazi ya jamii na watoto wao waweze kupatiwa elimu na huduma za Lishe ili kuelezea afua zinazolenga kuifikia jamii moja kwa moja kuweza kuishi kwa misingi ya lishe bora” amesema Dkt. Magembe
Dkt. Magembe ametoa rai kuwa mkazo Zaidi uwekwe hasa katika maeneo yenye chakula cha kutosha lakini bado kunachangamoto ya utapiamlo.
“Suala jingine ni elimu kwani imeonekana kwamba maeneo yenye chakula cha kutosha bado kunachangamoto ya utapiamlo hivyo elimu zaidi inahitajika ikiwemo uanzishwaji wa majiko darasa ambayo yatatumika katika kuelimisha jamii namna ya kuandaa vyakula vyenye lishe bora.” amesema Dkt. Magembe
Kwa upande wake mwakilishi kutoka UNICEF Ausmane Nang licha ya kuipongeza serikali kwa jitihada zilizofanyika katika shughuli ya mapitio ya sera ya chakula na Lishe ya mwaka 1992 amesema UNICEF itaendelea kuisaidia wizara katika kuhakikisha shughuli ya mapitio ya Sera inakamilika.