SHUKRANI KWA WAZIRI MKUU KUHAMASISHA MAZOEZI KUEPUKA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA
Posted on: May 16th, 2024UTEKELEZAJI WA BAJETI YA WIZARA YA AFYA 2023/24
Na WAF - Dodoma
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amempongeza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa kwa jitihada zake za kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi ili kujikinga na magonjwa Yasiyoambukiza.
Waziri Ummy ametoa pongezi hizo Bungeni Mei 13, 2024 akiwa anawasilisha hotuba yake ya bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2024/25 akielezea utekelezaji wa majukumu ya Wizara katika utoaji wa huduma za Kinga nchini.
"Kipekee nitumie fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa kwa kuwa mstari wa mbele kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi ili kudhibiti magonjwa Yasiyoambukiza ambayo yamekuwa yakiongezeka kila siku," amesema Waziri Ummy
Aidha, Waziri @ummymwalimu amesema katika kukabiliana na hali hiyo Serikali inaendelea kutekeleza mkakati wa Kitaifa wa Tatu wa kuzuia na kudhibiti magonjwa Yasiyoambukiza, Afya ya Akili na Ajali wa Mwaka 2021 - 2026 kwa kutekeleza afua kadhaa ikiwemo kuimarisha uratibu jumuishi kuanzia ngazi ya kijiji/mtaa mpaka Taifa.
"Tumejipanga kuongeza kasi ya elimu na uhamasishaji wa jamii kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza, Afya ya Akili na Ajali, kujengea uwezo mifumo ya utoaji wa huduma za Afya katika kufanya uchunguzi na matibabu ya magonjwa hayo pamoja na kuimarisha ufuatiliaji na tathmini wa afua hizo.
Pia, Waziri Ummy amesema ugonjwa Shinikizo la Juu la Damu uliongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi wa nje (OPD) kwa magonjwa Yasiyoambukiza (NCDs) wakichangia 26.1% sawa na wagonjwa 1,214,911 ikifuatiwa na ugonjwa wa Kisukari, 12.0% sawa na wagonjwa 559,597.
"Magonjwa mengine ya NCDs yaliyoongoza kwa OPD ni magonjwa ya Ngozi yakichangia kwa asilimia 8.3, ugonjwa wa Pumu asilimia 6.3 pamoja na magonjwa ya Macho asilimia 5.4." Amesema Waziri Ummy
Mwisho, Waziri Ummy amesema idadi ya wagonjwa wa nje waliohudhuria katika vituo vya kutolea huduma kutokana na magonjwa Yasiyoambukiza imeongezeka hadi kufikia wagonjwa 4,656,579 saw na 13% Mwaka 2023/24 ukilinganisha na Mwaka 2022/23 walikua wagonjwa 4,263,597 sawa na 12.8%.