Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI KUTANUA WIGO WA HUDUMA ZA UTENGAMAO.

Posted on: September 18th, 2024

Na WAF - Dar es Salaam.

Serikali inaendelea kutanua wigo wa huduma za Utengamao kwa kuanzisha vituo vipya katika Hospitali ambazo kwa sasa hazitoi huduma hizo hususani katika vituo vya huduma za afya ya msingi ili kuwafikia wahitaji hasa wale wanaoishi maeneo ya vijijini.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Aldof Mkenda akimuwakilisha Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama wakati wa ufunguzi Kongamano la pili la Utengemao linalofanyika Septemba 18, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Amesema Prof. Mkenda amesema Serikali imepanga kupanua idadi ya hospitali zinazotoa huduma bobezi za utengamao kwa kuanzisha Hospitali maalum ya utengamao katika mkoa wa Tabora ambayo itajumuisha pia huduma za wazee na Shufaa huku lengo likiwa ni kuendelea kuboresha huduma hizo.

“Kujumuisha na kuanza kutoa kwa huduma za utengamao katika Huduma za Afya ya Msingi kutafanya huduma hizi kupatikana zaidi kwa wahitaji hasa wale wanaoishi maeneo ya vijijini, itaambatama na kushughulikia pia upungufu wa rasilimali watu katika huduma za Utengamao hasa katika vituo vya afya ya msingi”. Amesema Prof Mkenda.

Aidha, Prof. Mkenda ameziasa Wizara za kisekta kuendelea kufanya kazi kwa pamoja kwa lengo la kuleta ustawi katika jamii.

“Serikali inaendelea kutilia mkazo elimu jumuishi kwa kuandaa mazingira wezeshi, ufundishaji na ujifunzaji wa watoto wenye changamoto mbalimbali kama walimu wanawezeshwa ili kuweza kutoa elimu inayokidhi mahitaji ya watoto hawa. Hivyo, huduma hizi za utengamao zinatakiwa kuendelea kutolewa si tu kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya pekee bali kwenye ngazi ya jamii na hata mashuleni”. Amesema Prof. Mkenda.

Pia Prof. Mkenda ametoa rai juu ya msisitizo wa Serikali wa kutaka mifumo ya kutolea huduma kusomana kwenye mfumo mama wa e-HMIS.