Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI KUENDELEA KUCHUKUA HATUA ZA KUDHIBITI NA KUTIBU KIFUA KIKUU

Posted on: October 6th, 2024

Na WAF - Siha, Kilimanjaro

Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kuchukua hatua za kudhibiti na kutibu ugonjwa wa Kifua Kikuu kwa kufanya tafiti kwa kushirikiana na Taasisi nyingine ndani na nje ya nchi.

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Oktoba 5, 2024 alipotembelea katika Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Magonjwa ambukizi Kibong'oto akiwa katika ziara yake katika Halmashauri ya Wilaya ya Siha Mkoani Kilimanjaro.

"Kiu ya Serikali ni kuendelea kufanya tafiti kwa kushirikiana na taasisi nyingine hata kama ni za Kimataifa ili tuweze kuoata tiba ambayo inauwezo wa kuwaponya haraka zaidi na mkaondokana na hii kadhia ambayo imeendelea kuchukua muda mrefu." Amesema Waziri Mhagama

Aidha, Waziri Mhagama amesema Jukumu la Serikali ni kuhakikisha Afya za wananchi zinaimarika ambapo amebainisha mikakati watakayokwenda kuifanya ikiwa ni pamoja na kufanya tafiti na kukutana na tasisi ambazo zimepewa jukumu la kuzuia maambukizi hayo ili ziendelee kutekeleza wajibu wake wa kutosha.

Waziri Mhagama amewahahakishia wagonjwa hao kuwa Serikali itaendelea kuwa karibu nao, haitachoka wala kuwaacha kuendelea kutoa huduma za Oxygen pamoja na kuboresha miundombinu ili kuendelea kusaidia kupumua na kuokoa uhai wao.

Wakati akiwa katika Zahanati ya Mahusiano Waziri Mhagama ameielekeza Halmashauri ya Wilaya ya Siha kujenga kichomeo taka haraka pamoja na sehemu ya kupumzikia ndugu wa wagonjwa ili Zahanati hiyo ianze kufanya kazi ndani ya wiki moja kutoka leo (Oktoba 12, 2024).

Waziri Mhagama yupo katika ziara Mkoani Kilimanjaro kwa muda wa siku Sita akiendelea kukagua na kuzindua miradi ya Sekta mbalimbali ikiwemo ya Sekta ya Afya ambapo leo ikiwa ni siku ya Pili.